Jamhuri ya Afrika ya Kati imeendelea kukumbwa na machafuko ambapo kwa
uchache watu watatu wameripotiwa kuuawa katika machafuko hapo jana.
Habari kutoka nchini humo zinasema kuwa, watu wenye silaha wamefanya
mashambulio katika vijiji kadhaa vya kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya
Afrika ya Kati. Aidha mashambulio hayo yaliambatana na wizi na uporaji
wa mali za wanavijiji.
Wanavijiji hao wameziambia duru za habari kwamba,
vikosi vya Umoja wa Afrika vilivyoko nchini humo MISCA havionyeshi
radiamali yoyote kuhusiana na mashambulio hayo. Hivi karibuni pia, Rais
Catherine Samba-Panza wa Jamhuri ya Afrika ya Kati alivikosoa vikali
vikosi vya kigeni vilivyoko nchini humo kutokana na kushindwa kwao
kuyapokonya silaha makundi ya wanamgambo yanayobeba silaha. Machafuko
katika Jamhuri ya Afrika ya Kati yanaendelea huku Waislamu wa nchi hiyo
wakiwa ndio wahanga wakuu wa machafuko hayo, kutokana na kuuawa na
wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka. Tokea mgogoro wa Jamhuri ya
Afrika ya Kati uanze mwezi Disemba mwaka uliopita, Waislamu wapatao laki
tatu na sitini elfu wa nchi hiyo wamekimbilia katika nchi jirani
zikiwemo za Cameroon na Chad.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment