Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Saturday, December 7, 2013

Utata kuhusiana na uhalali wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kusikiliza jinai za wanajeshi wa Misri

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imepokea maombi ya familia za wahanga wa machafuko yaliyotokea nchini Misri la kusikilizwa jinai zilizotendwa na Jenerali Abdul Fattah al Sisi, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, ingawa mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria wa kusikiliza kesi zilizowasilishwa na wananchi. Familia za wahanga wa machafuko ya Misri wametaka ifunguliwe kesi dhidi ya Jenerali al Sisi na maafisa wengine wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo  kwa kufanya  mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Muhammad Morsi kulikopelekea kuuawa maelfu ya wananchi wa Misri tarehe 14 Agosti mwaka huu.
Mahakama ya ICC imefikia uamuzi wa kusikiliza jinai hizo baada ya timu ya mawakili wa kimataifa kuwasilisha nyaraka na ushahidi mbele ya mahakama hiyo unaothibitisha kwamba serikali ya kijeshi ya Misri ilitenda jinai baada ya kuondoshwa madarakani Rais Morsi. Katika kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni, Misri imeshuhudia matukio mawili muhimu ya kijamii, ambayo ni uchaguzi na machafuko. Katika kipindi hicho cha miaka mitatu, wananchi wa Misri walishiriki kwenye chaguzi za bunge, madiwani na ule wa rais. Lakini hakuna hata uchaguzi mmoja kati ya chaguzi hizo ambao ulileta amani na utulivu huko Misri, bali zilisababisha kuzuka na kuongezeka machafuko zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Kwani katika chaguzi hizo, kwa mara ya kwanza kulishuhudiwa chama chenye mirengo ya Kiislamu kikijipatia ushindi. Suala hilo halikukuridhiwa na wala kuwafurahisha wanajeshi na  makundi ya kiliberali nchini humo. Hivyo, wale wanaojinadi kutetea demokrasia nchini Misri, walikanyaga misingi ya demokrasia na kufanya maandamano makubwa na hatimaye wanajeshi wakapata kisingizio cha kuupindua utawala huo uliochaguliwa na wananchi. Hatua hiyo iliyochukuwa na wanajeshi wa Misri, haikukubaliwa na wafuasi wa harakati ya Ikhwaanul Muslimiin na wapenda haki nchini humo, hivyo nao waliamua kufanya maandamano kwenye miji mbalimbali dhidi ya wanajeshi, maandamano yaliyosababisha kuuawa maelfu ya wananchi kwa  amri ya Jenerali al Sisi. Kitendo hicho cha wanajeshi wa Misri kimeonyesha wazi jinai zilizotendwa dhidi ya binadamu, jambo ambalo kukabiliana nalo ni miongoni mwa misingi ya kuundwa mahakama ya ICC. Mawakili wa kimataifa wameamua kufikisha maombi ya kufunguliwa mashtaka wanajeshi na hasa Jenerali al Sisi na baadhi ya viongozi wengine wa serikali ya mpito kwenye mahakama hiyo ya jinai, kutokana na kuwa  mahakama za Misri zinadhibitiwa na wanajeshi na mabaki ya utawala wa zamani wa dikteta kibaraka, Hosni Mubarak. Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC hivi sasa imekubali kusikiliza maombi ya wahanga wa ukandamizaji wa nchini Misri, ingawa katiba ya mahakama hiyo haitoi fursa ya kusikilizwa mashtaka yaliyofunguliwa na wananchi wa nchi hiyo. Imeelezwa pia kuwa, Mahakama ya ICC ina uwezo tu wa kusikiliza kesi za jinai zilizofanyika kwenye nchi mwanachama wa mahakama hiyo au pale Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapotoa amri kwa mahakama ya ICC kusikiliza kesi hizo.  Kwa kuzingatia kwamba Misri si mwanachama wa ICC, ni jambo lililo mbali kwa Baraza la Usalama kuweza kutoa idhini kwa mahakama hiyo kusikiliza jinai za wanajeshi wa Misri.

No comments: