Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa Jumanne hii liliidhinisha mipango ya kuongeza karibu mara mbili
idadi ya askari jeshi wa kulinda amani huko Sudan Kusini katika juhudi
za kuwalinda raia na machafuko huku taarifa za kugunduliwa makaburi ya
umati zikizusha hofu ya kutokea mapigano ya kikabila katika taifa hilo
changa zaidi duniani. Baraza la Usalama limesema limeidhinisha kutumwa
huko Sudan Kusini wanajeshi wengine elfu sita.
Nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa jana ziliidhinisha kwa sauti moja mpango wa Ban
Ki-moon Katibu Mkuu wa umoja huo wa kuimarisha nguvu za kikosi cha
wanajeshi wa kulinda amani huko Sudan Kusini kwa kuzidisha idadi ya
wanajeshi hadi 12,500 na polisi 1323. Umoja wa Mataifa unaongeza kiwango
hicho cha walinda amani huko Sudan Kusini huku raia wa nchi hiyo
wasiopungua elfu 45 wakiwa wamepata hifadhi katika vituo vya umoja huo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hata hivyo ametahadharisha kuwa walinda
amani hao hawataweza kumlinda kila raia anayehitaji msaada huko Sudan
Kusini licha ya kuongezwa kwa idadi hiyo ya askari wa kulinda amani.
No comments:
Post a Comment