Kundi la waasi wa M23 la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetishia
kulitwaa tena jimbo la Kivu kaskazini lililoko mashariki mwa nchi hiyo.
Waasi wa M23 wametishia kwamba watauteka tena mji wa Goma makao makuu
ya jimbo hilo, iwapo mazungumzo kati ya kundi hilo na serikali ya
Kinshasa yatavunjika. Afisa mmoja wa kundi la waasi wa M23 amefichua
kwamba, mji wa Goma utatekwa tena, kwa sababu serikali ya Kinshasa
haitaki kutekeleza matakwa yao.
Kiongozi huyo amesema kuwa, serikali ya Kongo badala ya kukidhi
matakwa ya waasi inakitegemea zaidi kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa
cha kukabiliana na makundi yenye silaha mashariki mwa nchi hiyo kwa
dhana kwamba kinaweza kutatua matatizo ya Kongo. Amesema kuwa, tokea
kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa kinachoundwa na nchi za Tanzania,
Afrika Kusini na Malawi kiingie nchini Kongo, serikali ya Kinshasa
imekuwa ikifanya jitihada za kuwalazimisha waasi wapokonywe silaha na
kutia saini makubaliano ya amani bila ya kufanyika mazungumzo.
No comments:
Post a Comment