Leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeadhimisha mwaka wa 25 tangu kuuawa
shahidi abiria wa ndege ya Shirika la Ndege la Iran Air ambayo
ilitunguliwa kwa makombora ya manowari ya kivita ya Marekani.
Katika hujuma hiyo ya kigaidi ndege ya abiria aina ya Airbus ya
Shirika la Ndege la Iran Air iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas, kusini mwa
Iran, na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa
makombora mawili kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi.
Manowari ya kijeshi ya
Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu
wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo wakiwemo wanawake na watoto
wachanga. Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama wa serikali ya
Marekani.
Kumbukumbu ya tukio hilo imefanyika leo kusini mwa Iran katika Ghuba
ya Uajemi na kuhudhuriwa na maafisa wa kijeshi katika balozi kadhaa za
kigeni nchini Iran. Katika ujumbe wake kwa hafla hiyo Mkuu wa Vikosi
vyote vya majeshi ya Iran Meja Jenerali Sayyid Hassan Firuzabadi ametaka
hatua zichukuliwe ili kuzuia kukaririwa tena jinai kama hiyo ya
Marekani.
Naye Brigedia Jenerali Farzad Esmaili kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa
Anga cha Iran amesema tukio la kutunguliwa ndege ya abiria ya Iran ni
dalili ya wazi kuwa Marekani inawahadaa walimwengu inapodai kutetea haki
za binaadamu. Kwa upande wake Jenerali Rahim Mumtaz mwambata wa kijeshi
wa Ubalozi wa Pakistan nchini Iran ambaye alizungumza kwa niaba ya
wambata wa kijeshi katika hafla hiyo amesema tukio la kutunguliwa ndege
hiyo ya Iran ni jinai kubwa ambayo inapaswa kulaaniwa na watu wote.
No comments:
Post a Comment