Marais wa nchi za Amerika ya Latini wamelaani hatua ya nchi kadhaa za
Ulaya ya kuzuia ndege ya Rais Evo Morales wa Bolivia kupaa kwenye anga
ya nchi zao na hivyo kuhatarisha maisha ya kiongozi huyo.
Marais wa Venezuela, Ecuador, Argentina, Uruguay na Suriname wamesema
Marekani ndiyo inayopaswa kulaumiwa kwani hakuna shaka kwamba nchi
zilizozuia ndege ya Morales zilipata mashinikizo kutoka Washington.
Rais Evo Morales alikuwa akitoka Russia baada ya kuhudhuria mkutano
wa kimataifa wa nishati na ndege yake ililazimika kutua kwa dharura
nchini Austria baada ya Ufaransa, Uhispania na Ureno kukataa kuiruhusu
ndege hiyo ipae kwenye anga yao.
Taarifa ya pamoja ya viongozi hao imetaka maelezo ya haraka kutoka
nchi hizo tatu za Ulaya kuhusiana na tukio hilo huku wakisema hatua hiyo
ya Paris, Lisbon na Madrid ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Rais wa
Bolivia ametishia kufunga ubalozi wa Marekani akisema Washington haina
heshima kwa mtu yeyote.
No comments:
Post a Comment