Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya IEBC imemzuia Bi.
Kethi Kilonzo, mwana wa kike wa waziri wa zamani nchini humo kuwania
kiti cha Seneta kwenye jimbo la Makueni baada ya kubainika kuwa,
hajatimiza masharti ya kugombea nafasi hiyo.
Jopo lililoundwa na IEBC kufuatilia kadhia hiyo limetoa uamuzi
likisema Bi. Kilonzo hajajiandikisha kama mpiga kura na hivyo hawezi
kugombea wadhifa huo. Kiti cha useneta cha Makueni kiliachwa wazi baada
ya kufariki dunia Mutula Kilonzo, baba yake Kethi Kilonzo, takriban
miezi miwili iliyopita.
Kethi alikuwa amepania kuwania kiti hicho kwa
muungano wa CORD unaoongozwa na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga. Hata
hivyo muungano huo umesema utapinga uamuzi huo wa IEBC katika Mahakama
Kuu na umesisitiza kwamba, Kethi ametimiza masharti yote ya kupiga kura
na hata kuwania wadhifa wowote wa uchaguzi.
Mbali na Bi Kilonzo, jopo la IEBC lilikuwa linamchunguza mgombea wa
muungano wa Jubilee ambapo limeamua kuwa, Bw. Philip Kaloki ametimiza
masharti yote na anaweza kugombea kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa
kufanyika baadaye mwezi huu.
No comments:
Post a Comment