Leo ni Jumatatu tarehe 29 Shaaban 1434 sawa na Julai 8, 2013.
Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, alifariki dunia Kim Il-sung
aliyekuwa Kiongozi na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti wa Korea
Kaskazini. Kim Il-sung alizaliwa mwaka 1912. Akiwa na cheo cha ukapteni
jeshini alirejea kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 1945 akiandamana na
jeshi. Alipanda ngazi ya uongozi haraka na akachaguliwa kuwa kiongozi wa
chama cha wakomunisti wa nchi hiyo. Mwaka 1948 wakati nchi hiyo
ilipoasisiwa na kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea Kim
Il-sung alifikia cheo cha uwaziri mkuu. Katika vita vya Korea Kim
Il-sung aliteuliwa kuwa kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo na mwaka
1972 akawa rais wa taifa hilo.
Miaka 57 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia
mtaalamu, mwanafikra na mwandishi wa Kitaliano Giovanni Papini.
Alizaliwa mwaka 1881 katika mji wa Florence nchini Italia. Giovanni
alipitia kipindi kigumu cha utoto na ujana wake. Hata hivyo hamu yake
kubwa ya masomo ilimpelekea kwenda katika maktaba za kijamii na
kuzidisha elimu na taratibu alidhihirisha uwezo wake mkubwa katika
taaluma ya fasihi. Msomi huyu ameandika vitabu vingi kama "A
man--finished," "The Failure," na “Life of Christ,"
Na siku kama ya leo miaka 1215 iliyopita alifariki dunia faqihi,
mtaalamu wa hadithi na mpokezi wa matukio ya kihistoria maarufu kwa jina
la Abu Naiim. Alizaliwa mwaka 130 Hijria nchini Iraq na anatambulika
kama mpokezi anayetegemewa na kuheshimiwa na maulamaa wa Kiislamu wa
hadithi. Ameandika kitabu cha As Salaat, na mwanahistoria maarufu Ibn
Nadim anasema kuwa, msomi huyo ameandika pia vitabu vya “al Manasik” na
“Masailul Fiqhi”.
No comments:
Post a Comment