Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, July 14, 2013

Jumapili, 5 Ramadhani 1434

Leo ni Jumapili tarehe 5 Ramadhani mwaka 1434 Hijiria, inayosadifiana na 14 Julai 2013 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 224 iliyopita mwafaka na leo, sehemu ya gereza la kihistoria la Bastille lilishambuliwa na kuharibiwa katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa na wananchi wa Paris. Jela hiyo ilijengwa mwaka 1369 kwa lengo la matumizi ya kijeshi. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa iligeuka na kuwa gereza la kutisha ambapo ndani yake walizuiliwa wafungwa wengi wa kisiasa hususan watu waliokuwa wakiendesha harakati za kudai jamhuri nchini humo.
Aidha gereza la Bastille lilidhihirisha udikteta wa wafalme wa Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita utawala wa kisultani ulipinduliwa huko Iraq katika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Abdul Karim Qassim na kuasisiwa utawala wa jamhuri nchini humo. Sultan Faisal wa Pili, mwana mfalme Abdallah aliyekuwa Naibu wa Sultan na Nouri Said Waziri Mkuu wa Iraq waliuawa katika mapinduzi hayo. Jenerali Abdul Karim Qassim ambaye alikuwa na misimamo ya kizalendo aliingia madarakani huko Iraq katika mapinduzi ya mwaka 1963 na kushika hatamu za uongozi baada ya kumuua Abdus Salaam aliyekuwa mtu wake wa karibu.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, alifariki dunia Mahdi Hamidiye Shirazi, malenga, mtafiti na mwandishi mkubwa wa zama hizo. Mahdi Shirazi alizaliwa mwaka 1293 Hijria katika mji wa Shiraz wa kusini mwa Iran na kutunukiwa shahada ya udaktari katika taaluma ya lugha na fasihi ya Kifarsi. Dakta Hamidi ameandika vitabu vingi vya mashairi ya Kifarsi, ambapo vingi vinahusiana na elimu ya mitindo, fasihi, historia na fani mbalimbali za mashairi.
Siku kama ya leo, miaka 20 iliyopita, alifariki dunia Dakta Abdul-Hadi Hairi, mmoja wa walimu wakubwa wa histori nchini Iran. Dakta Hairi, alizaliwa mjini Qum katika familia ya kidini. Aidha msomi huyo alikuwa mjukuu wa marjaa mkubwa na mwasisi wa hauza ya masomo ya kidini ya mjini hapo, Ayatullah Haj Sheikh Abdul-Karim Hairi.  Baada ya kusoma masomo ya awali ya theolojia, aliendelea na masomo yake huko nchini Canada.
Na siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, alizaliwa mjini Tabriz, Iran mmoja wa maulama wakubwa wa Kiirani, Haj Mulla Ali Alyaari Tabrizi. Haj Mulla Tabrizi alikuwa mtaalamu mkubwa katika fiq’hi, hadithi, mashairi na fasihi, huku akiwa na ujuzi pia katika fani ya tiba, mahesabu na nyota. Baada ya kusoma elimu ya dini huko mjini Najaf, Iraq, alirejea Iran na kujishughulisha na kufundisha na kuwalea wanafunzi.

No comments: