Leo ni Jumamosi tarehe 27 Shaaban mwaka 1434 Hijiria sawa na tarehe 6 Julai mwaka 2013 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Malawi
ilipata uhuru toka kwa Muingereza. Kabla ya uhuru ardhi hiyo ilikuwa
ikijulikana kwa jina la Nyasaland. Mwaka 1859, kundi wamisionari kutoka
Uskochi likiwa na mvumbuzi mashuhuri David Livingstone liliwasili nchini
Malawi. Mwaka 1891 Waingereza waliidhibiti nchi hiyo na kuiweka chini
ya himaya yao. Aidha mwaka 1953, Uingereza ikiwa na lengo la kuanzisha
umoja baina ya ardhi zilizokuwa chini ya udhibiti wake, ilianzisha
Shirikisho la Rhodesia na Nyasaland.
Ilikuwa mwaka 1962 wakati
kuliposhuhudiwa upinzani na maandamano makubwa ya kutaka kuvunjwa
shirikisho hilo. Hatimaye mwaka 1963 shirikisho hilo lilisambaratika na
mwaka uliofuata Nyasaland ikajipatia uhuru na kuitwa Malawi.
Miaka 38 iliyopita na katika siku kama ya leo, visiwa vya Comoro
vilivyoko barani Afrika vilipata uhuru. Karne kadhaa zilizopita kabla ya
hapo, visiwa hivyo vilivamiwa na kudhibitiwa na Waarabu. Ni katika
kipindi hicho ndipo wananchi wengi wa Comoro waliposilimu na kuingia
katika dini tukufu ya Kislamu. Kuanzia karne ya 16, kwa muda fulani
visiwa hivyo vilikaliwa kwa mabavu na Wareno, na mwaka 1842 sehemu ya
visiwa hivyo ikadhibitiwa na Ufaransa na taratibu ardhi yote ya Comoro
ikawa chini ya udhibiti wa mkoloni huyo. Baada ya mapambano ya miaka
kadhaa ya kupigania uhuru, hatimaye katika siku kama ya leo mnamo mwaka
1975, visiwa vya Comoro vilijikomboa na kupata huru.
Na siku kama ya leo miaka 51iliyopita aliaga dunia mwandishi wa
Kimarekani kwa jina la Faulkner William. Alizaliwa mwaka 1897. Faulkner
alirejea nchini kwake baada ya kushiriki katika Vita vya Kwanza vya
Dunia. Mwandishi William alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya
kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika
hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko
Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa
nchi hiyo. Riwaya za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika
sekta ya uandishi wa leo nchini Marekani.
No comments:
Post a Comment