Kiongozi wa upinzani nchini Misri Mohamed al Baradei, amekataa pendekezo
la kuwa waziri mkuu wa serikali ya mpito ya nchi hiyo. Mbali na kukataa
pendekezo hilo, Al-Baradei amependekeza wadhifa huo uchukuliwe na Ziyad
Bahaud-Din. Aidha kiongozi huyo wa upinzani, ametaka kuchukua wadhifa
wa naibu wa waziri mkuu katika masuala ya kisiasa. Hayo yanajiri katika
hali ambayo waungaji mkono wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin na Rais
aliyeenguliwa madarakani, Muhammad Mursi, wameendelea kufanya maandamano
mashariki mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Cairo na kutaka rais huyo
arejeshwe madarakani.
Mbali na hayo, waandamanaji pia wametaka aachiliwe
huru yeye na baadhi ya viongozi wa Ikhwanul Muslimin wanaoshikiliwa na
jeshi la nchi hiyo. Wakati huo huo jeshi la Misri limeweka doria kali
katika kila kona kwa lengo la kurejesha hali ya usalama nchini. Jana
Rais Vladimir Putin wa Russia alionya juu ya hatari ya machafuko
yanayoendelea nchini Misri kuwa yanaweza kuitumbukiza nchi hiyo kwenye
mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Rais Vladimir Putin amesema tayari
Syria imetumbukia vya kutosha katika vita vya ndani na kuwa jambo la
kusikitisha ni kuona hatari ya kutumbukia Misri katika mgogoro kama huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment