Muungano wa wapinzani nchini Misri NSF umetangaza wazi kwamba
hauna nia ya kufanya mazungumzo na Rais Muhammad Morsi na umekosoa
vikali hotuba ya kiongozi huyo aliyoitoa kwa mnasaba wa sherehe za
kukumbuka mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani.
Wapinzani hao wamesisitiza juu ya kufanyika maandamano makubwa tarehe
30 mwezi huu dhidi ya rais huyo. Mbali na mrengo huo kusisitizia
kufanya maandamano hayo ya siku ya Jumapili, pia umemtaka Rais Morsi
ajiuzulu na kutoa fursa ya kufanyika uchaguzi wa mapema.
Msemaji wa kambi hiyo Bwana Khalid Daud amekosoa tuhuma zilizotolewa
na Rais Morsi na kusema hazina msingi wowote. Daud ameongeza kuwa,
viongozi wa kambi hiyo nao watashiriki katika maandamano ya siku ya
Jumapili.
Wakati huo huo jumuiya ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Misri,
imelaani vikali mauaji ya kikatili yaliyofanywa na Masalafi wenye
misimamo mikali dhidi ya mwanazuoni maarufu wa Kishia Sheikh Hassan
Shehata na wafuasi wake wanne nchini Misri. Viongozi wa jumuiya hiyo
wamewaambia wanahabari kuwa, serikali imeshindwa kuwalinda raia wake
hususan wafuasi wa madhehebu ya Shia.
No comments:
Post a Comment