Miaka 1428 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, vita
vya Banil Mustalaq vilitokea. Bani Mustalaq lilikuwa kabila miongoni mwa
makabila ya Khaza'ah ambalo lilihamia katika vitongoji vya Makka.
Viongozi wa kaumu hiyo walikuwa wakiabudu masanamu na kueneza ibada hiyo
huko Makka. Banil Mustalaq walijiandaa kupigana vita na Uislamu baada
ya Waislamu kushika madaraka huko Madina. Kwa msingi huo, Mtume Muhammad
aliingia vitani pamoja na wafuasi wake kadhaa na kutoa pigo kubwa kwa
kabila hilo.
Miaka 32 iliyopita mwafaka na tarehe Saba mwezi Tir mwaka 1360 Hijria
Shamsiya, Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti aliuawa shahidi akiwa
pamoja na watu wengine 72 waliokuwa miongoni mwa shakhsiya bora wa
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya kuripuliwa kwa bomu ofisi kuu ya
chama cha Jamhuri ya Kiislamu. Ayatullah Beheshti pia alikuwa miongoni
mwa shakhsiya wa awali na waliotoa mchango mkubwa katika Mapinduzi ya
Kiislamu. Dakta Beheshti pia alikuwa mmoja kati ya wasaidizi wakuu wa
Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Mlipuko huo wa bomu uliwauwa
shahidi Dakta Beheshti na wasaidizi 72 wa Imam Khomeini wakiwemo
mawaziri na wabunge kadhaa.
Na siku kama ya leo miaka 7 iliyopita sawa na tarehe 28 mwezi Juni
mwaka 2006 jeshi la utawala wa Kizayuni lilianzisha mashambulio makubwa
dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza. Utawala wa Kizayuni uliendesha
mashambulio hayo ya kinyama kwa kisingizio cha kuuawa wanajeshi wake
wawili siku tatu kabla ya mashambulio hayo. Israel ilidai kuwa
wanamapambano wa Palestina walifanya oparesheni katika kituo kimoja cha
upekuzi na kuua wanajeshi wake wawili na kumkamata mateka mwingine
mmoja. Idadi kadhaa ya mawaziri, wabunge na wawakilishi wa baraza la mji
la serikali halali ya Palestina inayoongozwa na Hamas walitekwa nyara
na wanajeshi wa Israel katika siku za kwanza za mashambulizi hayo
makubwa ya jeshi yaliyopewa jina la "Mvua za Kiangazi". Mbali na hayo,
mamia ya raia madhlumu wa Palestina waliuawa shahidi na kujeruhiwa
katika mashambulizi ya kinyama ya anga na nchi kavu ya utawala wa
Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
No comments:
Post a Comment