Kagera. Watu sita wamefariki dunia wilayani Muleba mkoani Kagera
baada ya basi la abiria kupinduka katika ajali inayodaiwa kuwa ni
uzembe wa dereva ambaye alikuwa katika mwendo kasi huku akiongea na simu
ya kiganjani.
Ajali hiyo imetokea jana mchana katika mteremko wa
Kalonga Tarafa ya Kimwani wakati basi hilo likitokea Bukoba kwenda
Geita. Dereva wa gari hilo alifariki papo hapo katika ajali hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera,Philip Kalangi
alipotafutwa kutoa ufafanuzi wa ajali hiyo alisema atafutwe baadaye
kwani alikuwa anaelekea eneo la ajali.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Lembres Kipuyo alisema
taarifa za awali zinaonyesha kuwa dereva wa basi hilo alikuwa katika
mwendo kasi huku akiongea na simu na kuwa miongoni mwa abiria sita
waliofariki akiwamo mama na mtoto wake.
Wakati huohuo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’ amenusurika kifo baada ya gari lake kupata ajali maeneo
ya Katesh wakati akitoka Mbeya kwenda Arusha kushiriki mazishi ya
wafuasi wa Chadema waliofariki kwa mlipuko wa bomu.
Akizungumza kwa simu kutoka Kituo cha Polisi
Katesh, mbunge huyo alisema hakuna aliyekufa katika ajali hiyo
iliyohusisha gari lake na basi la Best Line linalofanya safari zake kati
ya Mwanza na Moshi.
Mashuhuda wa ajali hiyo walisema, gari la mbunge
huyo liliharibika upande wa kushoto alikokuwa amekaa kiongozi huyo
mwenye mvuto kwa vijana nchini.
Gari hilo aina ya Landcruiser lilikuwa likitokea
Mbeya wakati basi hilo la abiria likitokea Mwanza -kwenda Moshi huku
wakifuatana na kwa mujibu wa mashuhuda walipofika katika kona ya maeneo
ya Katesh kituoni , basi hilo lilikunja kona kuingia kituoni na ndipo
lilipogongana na gari la mbunge huyo wa Mbeya mjini kwa tiketi ya
Chadema.
Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Akili Mpwapwa amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuongeza kuwa uchunguzi bado unaendelea.
Sugu alikuwa akiwahi mazishi ya walifariki kwa bomu mjini Arusha, lililotokea Jumapili na kuua watu na kujeruhi wengine 36.
No comments:
Post a Comment