Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Jumapili ya leo
anatazamiwa kuelekea nchini Sudan kwa ajili ya mazungumzo yenye lengo la
kutatua mgogoro wa mafuta baina ya nchi hizo mbili.
Uhusiano wa pande mbili hizo ulizorota mwezi huu pale Sudan
iliposema itazuia mafuta ya Sudan Kusini kupita katika ardhi yake iwapo
wakuu wa Juba hawatasitisha uungaji mkono wao kwa waasi wanaoipinga
serikali ya Khartoum. Sudan Kusini inategemea mabomba ya Sudan kuuza
mafuta yake katika masoko ya kimataifa.
Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar anatazamiwa
kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Ali Osman Taha.
Waziri wa Mafuta wa Sudan Kusini Stephen Dhieu Dau pia ataandamana na
Machar mjini Khartoum. Mashirika ya mafuta ya China, India na Malaysia
ambayo hununua mafuta ya Sudan Kusini yanapata hasara kubwa kutokana na
mzozo baina ya nchi hizo mbili.
No comments:
Post a Comment