Maandamano makubwa yameanza leo nchini Misri ambapo kuna wasi
wasi wa kuibuka machafuko baina ya wafuasi na wapinzani wa Rais Mohammad
Morsi.
Waandamanaji hasimu walianza kukusanyika Jumamosi usiku kwa ajili ya
maandamano yanayofanyika katika kipindi hiki cha kuwadia mwaka mmoja
tokea Morsi achaguliwe kuwa rais wa Misri. Watu watatu tayari
wamesharipotiwa kupoteza maisha katika machafuko ya Jumamosi katika
maeneo kadhaa ya Misri.
Wapinzani wameitisha maandamano makubwa katika
medani ya Tahrir mjini Cairo kwa lengo la kumtaka Rais Morsi ajiuzulu.
Hata hivyo wafuasi wa Harakati ya Ikwanul Muslimin nao wameitisha
maandamano yao wakimuunga mkono Rais Morsi. Hali hiyo imeibua wasi wasi
wa uwezekano wa kuzuka machafuko na ghasia kote Misri katika maandamano
ya leo. Wapinzani wanataka Rais Morsi ajiuzulu na uchaguzi wa mapema
kuitishwa. Wanamlaumu kiongozi huyo kuwa amekengeuka mkondo wa mapinduzi
yaliyomtimua madarakani dikteta Hosni Mubarak. Uamuzi wa Mursi wa
kukata uhusiano na Syria na kuwaunga mkono magaidi nchini humo pia ni
jambo ambalo limewakasirisha Wamisri.
No comments:
Post a Comment