Hali ya mambo nchini Misri inaendelea kuharibika na inaonekana viongozi
wa nchi hiyo wanajiandaa kukabiliana na hali yoyote inayoweza kutokea
kutokana na kuongezeka malalamiko ya wananchi. Katika siku za hivi
karibuni Medani ya Tahrir kwa mara nyingine tena imekuwa uwanja wa
malalamiko ya wapinzani wa serikali ya Rais Muhammad Mursi wa nchi hiyo.
Kama ilivyokuwa wakati wa maandamano ya kupinga utawala wa dikteta
Husni Mubarack, wapinzani wa Mursi nao pia wamekuwa wakikesha kwenye
uwanja huo na kupiga nara za kupinga serikali yake.
Ripoti zinasema
mapigano yametokea kati ya askari usalama na wapinzani wa Mursi katika
mikoa mingine mitatu ya Dakahlia, Sharqiya na Gharbiya ambapo watu
wawili wameuawa na wengine 300 kujeruhiwa. Malalamiko na ghasia hizo
zinaripotiwa katika hali ambayo hivi karibuni Rais Mursi aliadhimisha
mwake wake wa kwanza tokea aingie madarakani ambapo alikiri kwamba kuna
baadhi ya makosa yaliyofanyika katika serikali yake katika kipindi hiki
na kuahidi kuyarekebisha. Wakati huohuo amependekeza kufanyike
mazungumzo ya kitaifa ili kuiondoa nchi hiyo kwenye mgogoro uliopo wa
kisiasa. Amependekeza kubuniwa kamati ambayo itajumuisha wawakilishi wa
vyama na makundi yote ya kisiasa na kisha kujadili na kuwasilisha
mapendekezo ya kutatuliwa matatizo hayo, jambo ambalo limepingwa vikali
na mrengo wa upinzani. Akizungumzia suala hilo, Ahmad Bahau Deen
Sha'ban, mratibu wa Jumuiya ya Kitaifa ya Mabadiliko ya Misri amesema
kwamba pendekezo la Rais Mursi la kubuniwa kamati ya kufuatilia na
kutatua makosa yaliyofanywa na serikali yake halina nia nzuri bali ni la
kimeonyesha tu na lisilokuwa na maana yoyote. Amesema pendekezo kama
hilo liliwahi kutolewa huko nyuma lakini halikufanyiwa kazi. Khalid
Dawoud, Msemaji wa Harakati ya Wokovu wa Kitaifa pia amekosoa matamshi
hayo ya Mursi na kuyataja kuwa yasiyo na tofauti yoyote na matamshi kama
hayo aliyotoa huko nyuma. Wapinzani wanasema kwamba matamshi ya hivi
karibuni ya Rais Mursi hayana kitu chochote kipya na kwamba hatua yake
ya kuwataka wapinzani anaowaita kuwa ni maadui wa demokrasia, washiriki
kwenye mazungumzo ya umoja wa kitaifa, imepitwa na wakati. Misimamo hiyo
ya pande mbili hasimu inachukuliwa katika hali ambayo wapinzani
wanasisitiza kwamba wameazimia kufanya maandamano ya kuadhimisha mwaka
mmoja wa mapinduzi ya Wamisri hapo siku ya Jumapili Juni 30. Aiman Nur,
mkuu wa Chama cha Ghad at-Thaura amesema kuwa amesikitishwa na matamshi
ya hivi karibuni ya Mursi na kusisitiza kuwa chama chake kitashiriki
katika maandamano hayo. Chama cha Wokovu wa Kitaifa ambacho ndicho chama
kikubwa zaidi cha upinzani nchini Misri kimewataka wananchi wote wa
nchi hiyo washiriki kwenye maandamano hayo. Wito huo unatolewa katika
hali ambayo jeshi la nchi hiyo limetoa taarifa likisema kuwa usalama wa
nchi hiyo uko hatarini na kwamba liko tayari kuchukua hatua ya kuulinda.
Kwa kuzingatia hali hiyo wataalamu wa mambo wanasema kwamba fursa ya
kulinda mapinduzi ya Misri, inaendelea kutoweka kwa kasi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment