Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amewataka maafisa wakuu serikalini kutumia nyadhifa zao kukabiliana na ufisadi.
Akizungumza wakati wa sherehe za kuapishwa Makatibu Wakuu wa wizara
mbalimbali hapo jana, Rais Kenyatta alisema ufisadi umelemaza serikali
zilizopita na kwamba hayuko tayari kufuata mkondo huo. Amesema serikali
yake inataka kufikisha maendeleo kwa mwananchi wa kawaida na ili
kufanikisha lengo hilo, sharti ulaji rushwa upigwe vita kwa nguvu zote.
Kuapishwa makatibu hao kunahitimisha mkwamo wa kisiasa ulikuwa
ukiripotiwa nyuma ya pazia kuhusu uteuzi wa maafisa hao. Uhuru amesema
sasa serikali iko tayari kuanza kazi ya kutekeleza ahadi alizotoa kwa
wananchi wakati wa kampeni.
Huku hayo yakijiri, Baraza la Mawaziri hapo jana liliwataka walimu
kusitisha mgomo wao wa kitaifa na kufanya mazungumzo na serikali ili
kutatua mivutano iliyoko. Mgomo wa kitaifa wa walimu wa shule za umma
umeingia siku yake ya nne leo Ijumaa huko nchini Kenya.
No comments:
Post a Comment