Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Wednesday, June 26, 2013

Iran yalaani mauaji ya Waislamu wa Kishia Misri

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Akbar Salehi amelaani jinai ya hivi karibuni iliyofanywa dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini Misri na kuonya kuhusu njama za kuibua machafuko ya kimadhehebu nchini humo. Katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Misri Mohamed Kamel Amr, Salehi alilaani mashambulizi ya kinyama yaliyofanywa na watu wanaokufurisha Waislamu wenzao dhidi ya Waislamu hao wa Kishia. Watu hao wenye misimamo mikali ya kasalafi walivamia nyumba ya mwanazuoni maarufu wa Kishia Sheikh Hassan Shehata na kuwaua shahidi Waislamu wanne wa Kishia, Juni 23.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amelaani kitendo hicho na kusema kuwa, nchi yake haitaruhusu watu wenye misimamo mikali kuchochea hitilafu za kimadhehebu nchini humo. Naye Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyed Abbas Araqchi amesema, maadui wanapanga kuyasababishia hasara mapinduzi ya Misri kupitia kuibua hitilafu za kimadhehebu. Amesema maadui awali walijaribu kuibua hitilafu baina ya Waislamu na Wakristo nchini Misri na sasa wameelekeza njama zao katika kuibua machafuko baina ya wafuasi wa madhehebu za Kiislamu. Nao wabunge wa Iran wametoa taarifa na kulaani mauaji ya Waislamu hao wa Kishia huko Misri baada ya kushambuliwa na watu wenye misimamo mikali ya Kisalafi. Wametoa wito kwa wanazuoni katika ulimwengu wa Kiislamu kutonyamazia kimya jinai hiyo. Wabunge wa Iran wamesema, Marekani ndiyo inayofaidika wakati inapotokea mizozo baina ya Waislamu duniani.

No comments: