Rais Barack Obama wa Marekani atawasili leo nchini Afrika Kusini
katika awamu ya pili ya safari yake barani Afrika. Akiwa nchini humo
Obama atakutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Jacob Zuma
na kushiriki kwenye mkutano wa waandishi wa habari.
Safari ya Rais wa Marekani barani Afrika ambayo itagharimu yapata
dola milioni mia moja, imegubikwa na hali mbaya ya kiafya ya rais wa
zamani wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela. Akiwa katika awamu ya
kwanza ya safari yake barani Afrika, Obama alisema mjini Dakar, Senegal
kuwa Mandela ni shujaa wa dunia ambaye iwapo atafariki dunia urithi wake
utabakia kwa kipindi cha muda mrefu.
Duru za ndani ya ikulu ya Marekani White House zinasema kuwa mipango
ya kukutana Barack Obama kama Rais wa kwanza mweusi wa Marekani na
Nelson Mandela kama rais wa kwanza mweusi katika historia ya kisiasa ya
Afrika Kusini imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara na watu wa familia wa
shujaa huyo wa Afrika. Obama aliwahi kukutana na Mzee Mandela mwaka 2005
alipokuwa Seneta katika Baraza la Seneti la Marekani pindi Mandela
alipokuwa safarini mjini Washington.
Tangu mwaka 2008 wakati Barack Obama alipoteuliwa kuwa mgombea urais
wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Demokrats, watu wa Afrika walikuwa
na matumaini makubwa na mwanasiasa huyo. Waafrika walitaraji kuwa, bara
lao hususan nchi za chini ya jangwa la Sahara, lingepewa kipaumbele
katika siasa za nje za Obama. Hata hivyo kiongozi huyo alikwenda kinyume
kabisa na matarajio ya Waafrika katika awamu ya kwanza ya uongozi wake
kati ya mwaka 2008 hadi 2012 na alilitembelea bara hilo mara moja tu kwa
kufanya safari nchini Ghana. Wakati huo walimwengu hususan watu wa
Kenya, walitaraji kwamba Obama ambaye ana asili ya Kenya, angetembelea
nchi hiyo, jambo ambalo halijafanyika hadi hii leo.
Weledi wa masuala ya siasa wanasema kuwa, safari ya sasa ya Rais
Obama wa Marekani barani Afrika ni fursa mwafaka ya kujaribu kuimarisha
satua ya Washington barani humo katika mipango ya muda mrefu ya
Marekani. Hususan ikitiliwa maanani kwamba, China na Brazil zinaongoza
kwa kuwa na satua kubwa zaidi ya kiuchumi na kisiasa barani Afrika na
sasa ni wakati wa Washington kufidia nakisi hiyo.
Kasi ya ustawi wa kiuchumi wa baadhi ya nchi za Kiafrika katika miaka
ya hivi karibuni imeifanya Marekani ilikodolee macho zaidi bara hilo.
Katika mtazamo huo Afrika Kusini ambayo ndiyo nguvu kubwa zaidi ya
kiuchumi na kisiasa barani Afrika, inapewa nafasi maalumu katika saisa
za nje za Marekani.
No comments:
Post a Comment