Jaji mmoja katika Mahakama Kuu ya Kenya anayechunguza mauaji ya
eneo la Tana Delta nchini humo ameshambuliwa na genge la wezi nyumbani
kwake.
Duru zinadokeza kuwa Jaji Bi. Grace Nzioka alikuwa akiendesha gari
karibu na nyumbani kwake katika mtaa wa Karen saa nne usiku jana
Jumatano wakati aliposimamishwa na genge la watu watano waliokuwa na
silaha nzito.
Jaji huyo ni mwenyekiti wa tume inayochunguza mapigano ya eneo la
Tana Delta ambapo zaidi ya watu 160 wameuawa katika kipindi cha miezi
sita iliyopita na maelfu ya wengine kuachwa bila makao.
Baada ya
kumchukua jaji huyo mateka, genge hilo liliingia nyumbani kwake na
kupora nyaraka kadhaa, laptop na televisheni. Polisi wanachunguza tukio
hilo na wanahoji ni kwa nini walinzi wawili wa jaji huyo hawakuwa
wamebeba silaha wakati wa tukio hilo. Mapigano katika eneo la Tana Delta
ni baina ya makabila mawili makuu hasimu ya Orma na Pokomo. Baadhi ya
duru nchini Kenya zinasema mapigano hayo yamechochewa na uamuzi wa
serikali ya Qatar wa kukodi ardhi zenye rotuba katika eneo hilo kwa
ajili ya kilimo.
No comments:
Post a Comment