Matokeo ya awali ya uchaguzi wa kabla ya wakati wa bunge la
utawala wa Kizayuni wa Israel yanaonyesha kuwa awamu nyengine mpya ya
mtikisiko na mvutano wa kisiasa na mizozano baina ya vyama inaujongelea
utawala huo haramu. Ripoti tofauti zinaonyesha kuwa chama cha Benjamin
Nentanyahu cha Likud kimeshindwa kupata ushindi mutlaki katika uchaguzi
huo. Matokeo ya awali ya uchaguzi wa bunge la Israel yanaonyesha kuwa
chama cha Likud kimepata ushindi mdogo dhidi ya wapinzani wake. Sambamba
na hayo chama kiitwacho Yisrael Beitenu "Israel Nyumba Yetu"
kinachoongozwa na Avigdor Lieberman na ambacho kilikuwa muitifaki wa
Likud katika uchaguzi huo nacho pia kimeshindwa kupata kura za maana,
hali ambayo inayumbisha nafasi ya muungano wa vyama hivyo viwili katika
uga wa kisiasa wa utawala wa Kizayuni.
Matokeo ya awali ya uchaguzi wa
bunge la utawala wa Kizayuni yanaashiria kuvurugika mahisabu ya kisiasa
aliyokuwa amepiga Netanyahu ya kuweza kujiimarisha zaidi kimadaraka
kupitia uchaguzi alioupigia upatu wa kabla ya wakati wa bunge la utawala
wa Kizayuni wa Israel. Matukio na mabadiliko ya kisiasa yanayojiri
ndani ya utawala wa Kizayuni yanaonyesha kuwa kutokana na kura
zilizopigwa kuna uwezekano mkubwa kwamba Shimon Peres, Rais wa utawala
huo ghasibu atampa kiongozi wa chama cha Likud Benjamin Netanyahu jukumu
la kuunda serikali mpya, hata hivyo kibarua kigumu mno kitamkabili
Nentanyahu hata kuweza kuifanikisha kazi hiyo. Kwa kuwa hakuweza kupata
ushindi wa kishindo alioutarajia, Netanyahu atalazimika kuunda serikali
ya muungano mkubwa wa vyama vyenye mielekeo tofauti ya mirengo ya kulia
na kushoto suala ambalo litazidi kuufanya uthabiti wa serikali hiyo uwe
tete na wa kulegalega. Ikiwa Netanyahu atashindwa kuunda serikali
kulingana na muda uliowekwa, Peres atakipa chama kingine jukumu la
kuitekeleza kazi hiyo. Na hivyo ndivyo ilivyotokea pia katika uchaguzi
uliopita wa bunge la 18 la utawala wa Kizayuni ambapo licha ya chama cha
Kadima kupata kura nyingi kilishindwa kuunda serikali kwa wakati
uliopangwa na matokeo yake ni kwamba chama cha Likud kinachoongozwa na
Netanyahu ndicho kilichounda serikali mpya licha ya kupata kura chache
kulinganisha na Kadima katika uchaguzi huo.
Alaa kulli hal matokeo ya uchaguzi wa kabla ya wakati wa bunge la
utawala wa Kizayuni sio tu yameigeuza kuwa jinamizi njozi aliyokuwa nayo
Benjamin Netanyahu ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo
lakini pia yanadhihirisha wazi kwamba utawala huo bandia sasa unaelekea
kwenye awamu mpya ya mtikisiko na hali ya mchafukoge wa kisiasa. Katika
hali kama hiyo haitaokuwa ajabu kwa serikali ijayo ya utawala wa
Kizayuni nayo pia kama aghalabu ya serikali zilizotangulia ikashindwa
kukamilisha kipindi cha miaka minne madarakani na kulazimika kuitisha
uchaguzi mwengine wa kabla ya wakati. Chaguzi za mara kwa mara za kabla
ya wakati katika utawala wa Kizayuni zinazidi kuonyesha kuwa giza totoro
na wingu zito limegubika anga ya mustakabali wa kisiasa wa utawala huo
haramu. Mtikisiko wa kisiasa ndani ya utawala wa Kizayuni
unaochanganyika na mazonge mengine ya ndani yakiwemo ya kiuchumi na
kijamii yanazidi kuizamisha Israel kwenye lindi la mgogoro na kuongeza
kasi ya mchakato wa kuporomoka na kusambaratika utawala huo haramu.../
No comments:
Post a Comment