Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amesema
kuwa, umoja wa Waislamu ndio utakaokuwa chimbuko la ushindi wao dhidi ya
njama mbalimbali za uistikbari na maadui. Ayatullah Muhammad Kashani
pia ametoa mkono wa baraka kwa kuwadia maadhimisho ya kuzaliwa mbora wa
viumbe Mtukufu Mtume wa Uislamu Muhammad al Mustafa (SAW), na
maadhimisho ya siku ya kuzaliwa mjukuu wa mtukufu huyo Imam Jaafar
Swadiq (as) na kuanza kwa Wiki ya Umoja. Amesema kuwa, Wiki ya Umoja ni
fursa muhimu ya kuimarisha umoja kati ya Waislamu wote kwa ujumla na
kwamba, mambo hayo ndiyo yatakayoweza kuzishinda njama za maadui.
Akiashiria kukaribia maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya
nchini Iran yaani tarehe 10 Februari, Ayatullah Muhammad Imami Kashani
amesisitiza kuwa, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, umekuwa
chachu ya kupatikana heshima na maendeleo katika kila sekta nchini Iran
hususan katika masuala ya sayansi na teknolojia na kuongeza kuwa, mwamko
na mapambano ya wananchi wa nchi za Kiarabu dhidi ya tawala za
uistikbari, nayo ni matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran.
Ameongeza kuwa, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa Iran,
nchi hii imegeuka na kuwa mtetezi mkuu wa Waislamu duniani na kwamba,
tofauti na misimamo hasi ya baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu,
Tehran imekuwa ndiyo muungaji mkono mkubwa kwa muqawama dhidi ya utawala
haramu wa Kizayuni katika eneo hili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment