Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, May 15, 2012

Utawala wa Kizayuni wa Israel waendelea kuchukiza duniani

Wimbi jipya la malalamiko na hasira dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel limeanza kushuhudiwa duniani.
Maandamano makubwa dhidi ya utawala haramu wa Israel yanaendelea katika nchi mbali mbali duniani kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kuanza kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na kuasisiwa utawala bandia wa Israel. Watu wa Palestina wanaitaja siku hiyo kuwa 'Siku ya Nakba' au Siku ya Nakama yaani maafa.


Kati kati ya mwezi Mei mwaka 1948, utawala haramu wa Israel uliundwa baada ya Wazayuni kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Baada ya kupita zaidi ya miongo sita tokea uundwe utawala wa Kizayuni, bado utawala huo haujaweza kuhalalisha uwepo wake bandia licha ya kutumia kila aina ya ujanja. Maandamano yanayoendelea duniani dhidi ya Wazayuni ni dalili ya wazi kuwa walimwengu hawautambui utawala huo ghasibu.
Hivi sasa maandamano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yanashuhudiwa hata katika nchi za Ulaya ambazo watawala wake ni kati ya waungaji mkono wakubwa wa utawala huo. Kwa mfano wakaazi wa London nchini Uingereza walijitokeza kwa wingi katika maandamano yaliyofanyika hivi karibuni kwa ajili ya kuwaunga mkono Wapalestina na kuupinga utawala wa Kizayuni.
Katika maandamano hayo ya Jumapili mjini London, wananchi wa Uingereza waliutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe mauaji ya wananchi wa Palestina mara moja.
Waandamamanji hao walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na maandishi ya kutaka uhuru wa ardhi za Palestina. Aidha walilaani vikali ukatili na unyama unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na hatia Palestina.
Kuanzia mwaka 1948 hadi sasa kila mwaka kati kati ya mwezi Mei katika siku ya kukumbuka kuundwa utawala bandia wa Israel, watu wa Palestina na wapenda uhuru kote duniani huandaa maandamano ya kutetea taifa linalodhulumiwa la Palestina.
Kwa kuzingatia nafasi ya serikali ya wakati huo ya Uingereza katika kuasisi utawala bandia wa Israel, watu wa matabaka mbali mbali Uingereza hasa Waislamu na wanaharakati wa masuala ya kijamii, wameandamana mbele ya ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza ambapo wamemtaka aushurutishe utawala wa Kizayuni ukomeshe kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na ukandamizaji unaofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina. Katika upande mwingine, wananchi wa Sweden pia wameandamana kuunga mkono Wapalestina kwa mnasaba wa 'Siku ya Nakama'. Maandamano pia yameripotiwa huko Uhispania katika mji wa Madrid. Kwa hakika maandamano haya yanaonyesha kuwa walimwengu wanawaunga mkono watu wanaodhulumiwa Palestina na kwa hivyo kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo utawala wa Kizayuni unavyoendelea kutengwa kimataifa.

No comments: