Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, April 22, 2012

Wanasiasa Tanzania watofautiana kuhusu tamko la Rais Kikwete la kupinga mjadala kuhusu muungano

Bi. Celina Kombani
Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba wa Tanzania, Celina Kombani amesema kuwa anaunga mkono tamko la Rais Jakaya Kikwete kwamba maoni ya kuvunjwa muungano hayatapewa umuhimu na tume ya kuandaa rasimu ya katiba mpya. Akizungumza na Radio Tehran kwa njia ya simu, Bi. Kombani amesema mchakato wa kuvunjwa muungano ni tofauti kabisa na masuala ya katiba. Hata hivyo Mbunge Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ndiye Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba ametofautiana na Waziri Kombani akisema kuwa Watanzania ndio wanaopaswa kuamua iwapo wanautaka muungano uendelee kuwepo au la. Kwa upande wake Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Wananchi CUF, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba ametetea tamko hilo la Rais Kikwete na kuongeza kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni matunda ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Wakizungumza kwa wakati mmoja na idhaa hii kwenye mahojiano maalumu, watatu hao wamesema mchakato wa kutafuta katiba mpya ni zoezi la kihistoria na wametoa wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu na kutoa maoni yao bila woga. Wamesisitiza kuwa Katiba mpya ndiyo chambo pekee cha kufikia mageuzi kamili ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

No comments: