Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, April 15, 2012

Vikwazo dhidi ya Iran, kutoka tishio hadi fursa

Marekani na waitifaki wake katika kipindi cha miezi michache iliyopita walianza kutekeleza vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu miaka 33 iliyopita. Kisingizio chao cha vikwazo hivi ni kujaribu kuishinikiza Iran isitishe harakati zake za nyuklia zenye malengo ya amani. Marekani na serikali za Umoja wa Ulaya zinadai kuwa mpango wa nishati ya nyuklia wa Iran unalenga kutengeneza bomu la nyuklia. Hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza bayana kuwa kujipatia silaha za nyuklia ni jambo ambalo linaenda kinyume kabisa na mafundisho ya kidini. Aidha Iran inasema kuwa kwa mtazamo wa kisiasa na kijeshi, silaha za nyuklia haziifanyi nchi iwe na nguvu. Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Iran kwa mara kadhaa wameashiria nukta hii kuwa uungaji mkono wa wananchi ndio chanzo kikubwa zaidi cha nguvu za mfumo wa Kiislamu wa Iran. Ikumbukwe kuwa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshatoa fatwa ya kutangaza kuwa haramu utengenejzaji silaha za nyuklia.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imependekeza eneo la Mashariki ya Kati lisiwe na silaha za nyuklia na tayari imewasilisha suala hili katika vikao vya kieneo na kimataifa. Ili kuthibitisha malengo yake ya amani, Iran imewaalika wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA katika vituo vyake vyote vya nyuklia. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Utengenezaji na Usambazwaji Silaha za Nyuklia NPT na hadi sasa haijakiuka sheria za IAEA. Pamoja na hayo Marekani kwa kupenyeza ushawishi wake katika wakala wa IAEA na kuwasilisha nyaraka bandia na za uongo imejaribu kuonyesha kuwepo mpango wa kijeshi katika miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani. Marekani imetumia vibaya ushawishi wake na kupelekea faili la nyuklia la Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuwasilishwa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Iran yakataa kusalimu amri mbele ya vikwazo

Marekani, Ufaransa na Uingereza zimetumia uwezo wao katika baraza hilo kupitisha maazimio kadhaa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo kati ya mengine, Iran imewekewa vikwazo vya kiuchumi. Lakini si tu kuwa vikwazo hivyo havijazuia mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani, bali pia vimeifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na irada imara zaidi ya kuendeleza mpango wake wa nyuklia. Lililo wazi ni kuwa, Marekani na waitifaki wake wa Ulaya kwa kupitisha maazimio kadhaa katika baraza la usalama wameshindwa katika malengo yao ya kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi. Baada ya kufeli, wameiwekea Iran vikwazo vya upande mmoja nje ya fremu ya Umoja wa Mataifa. Kutokana na kuwa mafuta ghafi ya petroli ndio chanzo muhimu zaidi cha pato la fedha za kigeni Iran na kutokana na kuwa Banki Kuu ya Iran ina nafasi muhimu katika mfumo wa biashara nchini, Wamagharibi wamejaribu kuweka vikwazo vikali zaidi katika sekta hizo mbili. Mashinikizo haya makali ya kiuchumi yanalenga kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ijisalimishe mbele ya matakwa haramu na ya kibeberu ya Marekani na waitifaki wake. Marekani imezishawishi serikali za Ulaya zisinunue mafuta ghafi ya Iran na ziisusie Banki Kuu ya Iran. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa ikiuza asilimia 18 ya mafuta yake katika nchi za Umoja wa Ulaya. Wanunuzi wakubwa zaidi wa mafuta ya Iran barani Ulaya walikuwa ni Ugiriki, Uhispania na Italia. Wamagharibi walikuwa wakidhani kuwa, kwa kutonunua mafuta ya Iran wangeudhuru vibaya uchumi wa nchi hii.

 Vikwazo vyadhuru Wamagharibi

Kabla hata ya vikwazo vya mafuta kuudhuru uchumi wa Iran, habari tu za vikwazo hivyo vilipelekea kuongezeka bei ya mafuta duniani. Jambo hilo limeathiri vibaya chumi za Ulaya. Bei ya mafuta yaliyosafishwa ya petroli katika aghalabu ya nchi za Ulaya imeongezeka kwa kiwango kisicho na kifani na kuibua hasira miongoni mwa wananchi katika nchi hizo zinazokumbwa na mgogoro wa kiuchumi.
Nukta ya kuzingatia ni kuwa hata kabla ya nchi za Ulaya kuanza kutekeleza vikwazo dhidi ya Iran; ni Iran ndiyo iliyochukua hatua ya kwanza ya kusitisha uuzaji wa mafuta yake kwa nchi hizo na hivyo kuzizidishia matatizo ya kiuchumi. Athari mbaya ya hatua ya nchi za Ulaya kuiwekea Iran vikwazo ni jambo ambalo kwa mara nyingine limethibitisha nafasi muhimu ya Iran katika soko la nishati duniani.
Katika ulimwengu ambao kutegemeana kati ya wanaotumia na wanaozalisha nishati kunazidi kuongezeka, katika ulimwengu ambao utandawazi wa uchumi umeleta misingi mipya ya kiuchumi kwenye mlingano wa kisiasa na kiuchumi duniani na katika uliwmengu ambao madola mapya yenye uwezo yameibuka kimataifa; vikwazo haviwezi tena kutumika kama chombo cha mashinikizo.
 
Historia ya vikwazo
Katika kipindi cha historia ya miaka mia na hamsini iliyopita hii itakuwa mara ya tatu kwa sekta ya mafuta ya Iran kukumbwa na vikwazo. Vikwazo vya kwanza viliwekwa na shirika la British Petroleum au BP wakati setka ya mafuta ya Iran ilipotaifishwa mwaka 1951. Mara ya pili kwa sekta ya mafuta ya Iran kuwekewa vikwazo ni punde baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979. Katika kipindi hicho Marekani ilisusia kununua mafuta ya Iran. Wakati huo Marekani ilikuwa ikinunua takribani mapipa laki sita ya mafuta ghafi kutoka Iran. Katika vipindi hivyo vyote viwili, Iran ilifanikiwa kwa kipindi cha muda mfupi kupata wanunuzi mbadala wa mafuta yake. Uzoefu wa muda mrefu unaonyesha kuwa vikwazo havijaathiri sana uhai wa kiuchumi wa Iran.
Hivi karibuni Umoja wa Ulaya ulitangaza vikwazo vya kutonunua mafuta ghafi ya petroli kutoka Iran. Vikwazo hivyo vimetangazwa katika hali ambayo mlingano wa kisiasa na kiuchumi duniani unatafautiana sana na ule wa karne iliyopita.
Mafanikio makubwa ya kiuchumi katika nchi zinazostawi za bara Asia ni jambo ambalo limepelekea kuibuka nchi mpya tajiri kiviwanda jambo ambalo limebadili mlingano wa kisiasa na kiuchumi duniani. Kwa hakika Marekani na nchi kubwa za Umoja wa Ulaya zimepoteza nafasi kama soko kubwa la nishati duniani. Hivi sasa kumeibuka nchi tajiri katika bara Asia ambazo sasa zinanunua kwa wingi mafuta ghafi ya petrol duniani. Isisahaulike kuwa Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya zinakumbwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi ambao bado haujaweza kutafutiwa ufumbuzi. Kwa hivyo, ongezeko la bei ya mafuta kufuatia vikwazo dhidi ya Iran ni jambo ambalo kati ya mengine litaathiri vibaya chumi za nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani.
Nukta nyingine ambayo tunaweza kuiashiria kuhusu hatua ya Marekani na Umoja wa Ulaya kuiwekea Iran vikwazo vya mafuta ni mtazamo wa wananchi na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu vikwazo hivyo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu sasa imekuwa ikikabiliwa na vikwazo mbali mbali. Katika kipindi hicho chote, Iran imejifunza vizuri namna ya kubadilisha vikwazo hivyo kuwa fursa kwa maslahi yake.
 
Iran yabadilisha vikwazo kuwa fursa
Miaka michache iliyopita, nchi za Kimagharibi ziliwashinikiza wauzaji wa mafuta yaliyosafishwa ya petroli wasiiuzie Iran mafuta yao. Lengo lao lilikuwa ni kuibua malalamiko ya wananchi wa Iran dhidi ya serikali na kwa njia hiyo waweze kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu. Katika kipindi hicho, Iran ilikuwa ikinunua nje ya nchi asilimia 40 ya mafuta ya petrol yaliyosafishwa pamoja na kuwa ilikuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta ghafi ya petroli. Kutokana na kuongezeka idadi ya magari yaliyokuwa yakizalishwa humu nchini, kiwango cha utumizi wa mafuta ya petrol kilitazamiwa kuongezeka. Marekani na Nchi za Ulaya ziliyashinikiza mashirika ya kimataifa yasiiuzie Iran mafuta yaliyosafishwa ya petroli. Lakini kinyume na walivyotarajia Wamagharibi, Iran haikusalimu amri, bali katika kipindi cha muda mfupi serikali ilianzisha mpango wa kutumia petrol kwa njia sahihi. Sambamba na hilo Iran ilijenga viwanda kadhaa vya kusafisha mafuta ghafi ya petroli na kwa muda mfupi Iran ikageuka kuwa muuzaji nje wa petroli iliyosafishwa. Kimsingi ni kuwa Iran imekuwa ikivigeuza vikwazo na kuvifanya kuwa fursa ya kujiimarisha na kujitegemea. Kwa hivyo kutokana na mshikamano uliopo kati ya wananchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vikwazo vya hivi karibuni vya Marekani na Umoja wa Ulaya vitatumika kuimarisha uwezo wa kujitegemea nchi hii.

Vikwazo havitazuia ustawi wa Iran

Iran inaelekea katika mkondo wa ustawi na hata visima vyake vya mafuta vikifungwa, nchi hii inaweza kujidhaminia mahitaji yake. Na kama alivyosema Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hata kama Wamagharibi hawatanunua kabisa mafuta kutoka Iran kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, nchi hii ina fedha za kigeni za kujitosheleza katika kipindi hicho na njama za maadui dhidi yake zitagonga mwamba tu. Lililo wazi ni kuwa pamoja na kuwepo njama za Wamagharibi wakiongozwa na Marekani; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia kuwa katika kipindi cha miaka 20 ijayo, kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, itageuka na kuwa dola lenye nguvu kubwa zaidi katika Mashariki ya Kati kwa mtazamo wa kisayansi na kiuchumi.
 

No comments: