Mtu mmoja amefariki dunia na wanachama wengine saba wa kundi linalotaka kujitenga eneo la pwani mwa Kenya la Mombasa Republican Council (MRC) baada ya kupigana na polisi nje ya Mahakama ya Sheria mjini Mombasa.
Mapigano hayo yalitokea baada ya polisi kuwazuia wanachama wa kundi hilo lililopigwa marufuku kuingia katika mahakama hiyo iliyokuwa ikisikiliza kesi inayohusu wanachama wa MRC. Vijana wa kundi hilo linalotaka kujitenga pwani ya Kenya waliokuwa wamevaa tisheti zenye maandishi "Pwani si Kenya", walijaribu kuingia mahakamani kwa nguvu lakini wakazuiwa na polisi wa kuzuia ghasia.
Serikali ya Kenya imelipiga marufuku kundi hilo na imetangaza kwamba haitafanya mazungumzo na watu wanaotaka kujitenga.
Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga alisema jana kwamba serikali ya Nairobi haitafanya mazungumzo na kundi hilo hadi pale litakapotupilia mbali kaulimbiu yake ya "Pwani si Kenya" na kujitambua kuwa ni Wakenya.
No comments:
Post a Comment