Huku makundi hasimu ya Sudan Kusini yakijiandaa kwa duru
mpya ya mazungumzo ya amani mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Salva Kiir
Mayardit ametoa wito wa kufanyika maridhiano ya kitaifa ili kuinusuru
nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. Akilihutubia bunge la taifa, Rais
wa Sudan Kusini amesema pana haja ya pande zote hasimu kusameheana na
kushikana pamoja ili kuijenga nchi. Amewataka wananchi wote kuisaidia
serikali yake kudumisha umoja wa kitaifa. "Sina kinyongo wala hasira
dhidi ya mtu yeyote hata wale ambao hatuafikiani katika masuala kadhaa.
Tunaweza kuketi na kujadiliana masuala yaliyopo na hatimaye kutatua
tofauti zetu kwa maslahi ya taifa" amesema Rais Kiir ambele ya wabunge
wa nchi yake.
Mwito wa rais Salva Kiir unakuja siku chache baada ya Riek
Machar, kiongozi wa waasi na makamu wa zamani wa rais wa Sudan Kusini
kusema kuwa yuko tayari kushiriki kwenye mchakato wa maridhiano ya
kitaifa kwa lengo la kuzuia umwagikaji zaidi wa damu nchini mwake. Dkt
Machar amenukuliwa akisema, uwezekano upo kwa yeye kusaini makubaliano
ya kudumu ya amani kati yake na Rais Salva Kiir. Hii ni katika hali
ambayo, Jumatano ya hapo kesho Juni 4 kunatarajiwa kufanyika duru
nyingine ya mazungumzo kati ya wajumbe wa serikali ya Juba na wale
wanaomuunga mkono Dk. Riek Machar huko Addis Ababa, Ethiopia. Mazungumzo
hayo yamekuwa yakisimamiwa na Jumuiya ya Kieneo ya IGAD ambapo mwezi
uliopita wa Mei, kwa mara ya kwanza tangu kuzuka machafuko Sudan Kusini,
Rais Salva Kiir alikutana ana kwa ana na hasimu wake Dk. Machar na
kusaini makubaliano ya usitishwaji vita. Hata hivyo makubaliano hayo
yalikiukwa saa chache tu baada ya kusainiwa, huku kila upande
ukiunyooshea kidole cha lawama upande wa pili na kusema ndio uliokiuka
makubaliano hayo. Licha ya hayo yote, Rais Salva Kiir amesema, ujumbe wa
serikali yake utakwenda Addis Ababa ukiwa na nia njema na irada thabiti
ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Sudan Kusini.
Ingawa kuna kauli za kutia matumaini kutoka kwa viongozi wa
pande zote hasimu katika mgogoro wa Sudan Kusini, lakini hali halisi ya
mambo ni kinyume kabisa na kauli hizo. Umoja wa Mataifa umetahadharisha
kuwa, kuna hatari ya kuzuka hali mbaya ya kibinadamu Sudan Kusini iwapo
mapigano hayatasitishwa. Hii ni katika hali ambayo, ripoti zinaonyesha
kuwa mgogoro huo umeendelea kushika kasi katika siku za hivi karibuni na
kwamba raia zaidi wanaendelea kukimbia makazi yao. Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa wiki iliyopita lilipitisha azimio linalotaka
kurejeshwa amani na utulivu haraka iwezekanavyo huko Sudan Kusini.
Takwimu zinaonyesha kuwa, tangu kuzuka mapigano Disemba 15
mwaka uliopita, zaidi ya wakimbizi 300,000 kutoka Sudan Kusini
wamekimbilia katika nchi za Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda.
Taasisi mbalimbali za kutetea haki za binadamu ikiwemo
Kamisheni Kuu ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa zimekemea
ukiukwaji wa haki za binadamu na jinai za kivita zilizotendwa na pande
zote husika kwenye mgogoro wa Sudan Kusini.
Wachambuzi wengi wanafuatilia kwa karibu duru mpya ya
mazungumzo kati ya serikali ya Juba na upande wa Riek Machar
yanayotarajiwa kuanza kesho nchini Ethiopia, ili kuona kama kauli za
matumaini walizotoa mahasimu hao wa kisiasa zitaambatana na vitendo kwa
lengo la kukomesha kabisa mapigano Sudan Kusini.
No comments:
Post a Comment