Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: kushikamana
na Qur'ani ni jambo ambalo litauletea Umma wa Kiislamu heshima.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo Jumanne hapa
mjini Tehran wakati alipokutana na mjumuiko wa maustadhi, maqarii na
mahufadh walioshiriki katika Mashindano ya 31 ya Kimataifa ya Qur'ani
Tukufu. Ameongeza kuwa, lengo la juu la kuihifadhi na kuisoma Qur'ani
Tukufu ni 'kufahamu na kutekeleza' maamrisho yake sambamba na
'kufungamana na maneno ya Mwenyezi Mungu. Kiongozi Muadhamu ameongeza
kuwa: "Uongofu wa Mwenyezi Mungu" na "Kufahamu vigezo vya kimsingi vya
Qur'ani katika masuala muhimu kama vile kumfahamu ipasavyo adui" ni kati
ya nukta muhimu za kufungamana na Qur'ani.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema tatizo kubwa zaidi la ulimwengu
wa Kiislamu ni kujiweka mbali na mafundisho ya Qur’ani Tukufu na natija
ya hilo imekuwa ni kughafilika Waislamu kuhusu njama na ukhabithi wa
maadui wa Uislamu. Ameongeza kuwa njia ya kufidia upungufu huu wa
kimsingi katika ulimwengu wa Kiislamu ni kufahamu kwa kina vigezo
vilivyowekwa katika Qur'ani Tukufu. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa,
sera za maadui wa Uislamu zimejengeka katika msingi wa kuzusha vita vya
ndani kupitia vibaraka na kusababisha ndugu wauane wao kwa wao katika
jamii za Kiislamu. Ameongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kuna
baadhi ya watu katika Umma wa Kiislamu hawafahamu hizi sera sumu za
maadui bali hata wako tayari kumpa shetani mkono na kushirikiana na hata
utawala wa Kizayuni wa Israel katika kukabiliana na ndugu zao Waislamu.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameongeza kuwa, maadui wa
Uislamu walizidisha njama zao dhidi ya Uislamu baada ya ushindi wa
Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu ameashiria namna vijana wa Iran walivyoikumbatia kwa wingi
Qur'ani Tukufu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema, hiyo
ni neema kubwa. Ameongeza kuwa, kufungamana na Qur'ani kunaikaribisha
jamii katika mafundisho yaliyojaa uhai ya kitabu hicho kitukufu na
kwamba hilo ndilo lengo kuu na la juu katika kuhifadhi na kuisoma
Qur'ani Tukufu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea
kusema kuwa: "Kwa kufungamana na Qur'ani, umma wa Kiislamu unaweza
kuelekea katika izza ambayo Mwenyezi Mungu SWT amewaahidi."
Mashindano ya 31 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yalimalizika jana
hapa Tehran baada kufanyika kwa muda wa wiki moja. Mashindano hayo
yalianza tarehe 27 Rajab katika mkesha wa maadhimisho ya kubaathiwa
Mtume Muhammad SAW. Mashindano hayo yalikuwa na maqarii na mahufadh 120
wa Qur'ani Tukufu kutoka nchi 75 duniani huku kukiwa na jopo la majaji
15 ambapo 10 kati yao ni kutoka nchi za kigeni na watano ni Wairani.
No comments:
Post a Comment