Jiji la London, Uingereza ni mwenyeji wa mkutano wa kimataifa
unaojadili vitendo vya ubakaji vinavyotokea vitani katika maeneo
mbalimbali duniani. Mkutano huo wa kimataifa umeanza shughuli zake leo
na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 117. Taarifa zinasema kuwa,
imetolewa protokali ya kimataifa kwenye mkutano huo yenye lengo la
kuchunguzwa jinai na ubakaji wakati wa vita na kufuatiliwa kisheria
watenda jinai hizo.
Phumzile Mlambo-Ngcuka Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mataifa
anayeshughulikia masuala ya wanawake amesema kuwa, ijapokuwa wanaume
hubakwa kwenye maeneo ya vita, lakini wanawake ndiyo wahanga wakubwa
zaidi wa jinai hizo kwani karibu asilimia 70 ya wanawake huwa walengwa
wakuu wa vitendo hivyo vya ubakaji wakati vinapotokea vita katika maeneo
mbalimbali duniani. Washiriki wa mkutano huo wameonyesha matumaini ya
kupatikana njia zitakazoweza kukabiliana na vitendo hivyo vichafu, na
kutekelezwa haki na usawa kwa wahanga wa vitendo hivyo.
Katika miaka ya hivi karibuni, wanawake katika nchi za Bosnia
Herzegovina, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Somalia walikuwa
waathirika wakubwa wa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia.
Nchini Bosnia Herzegovina ambapo wanawake wasiopungua elfu hamsini
walibakwa wakati wa vita, na watendaji wa jinai hizo bado
hawajachukuliwa hatua zozote za kisheria licha ya kupita miongo miwili
sasa. Vitendo vya ubakaji dhidi ya wanawake wakati wa vita siyo jambo
jipya katika zama hizi, lakini kasi ya vitendo hivyo vichafu inazidi
kutia wasiwasi mno. Jambo la kusikitisha ni kwamba vitendo hivyo vichafu
vinaonekana kuwa jambo la kawaida, na hadi sasa hakuna mikakati yoyote
ya maana iliyowekwa kukabiliana na vitendo hivyo au hatua zinazopaswa
kuchukuliwa dhidi ya watenda jinai hizo.
Alaa kulli haal, wanawake ndiyo waathirika wakubwa wa vitendo vya
ubakaji ikilinganishwa na wanaume wakati wa vita, ambapo katika Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo pekee, kila siku wanawake na wasichana 36
hubakwa, na idadi ya waathirika wa vitendo hivyo ni zaidi ya wanawake
laki mbili kutokea mwaka 1998. Hata hivyo, viongozi, vyombo vya upashaji
habari, taasisi na mashirika ya kieneo na kimataifa wamekuwa na
uzingatiaji mdogo katika masuala hayo. Na hasa ikizingatiwa kwamba,
waathirika wa vitendo vya ubakaji wakati wa vita hupatwa na machungu
makubwa ikilinganishwa na wa makundi mengine kama yale yanayokabiliwa na
mateso ya kimwili na kiakili. Kwa minajili hiyo, mkutano huo
unaohudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 117 duniani ili kujadili vitendo
vya ubakaji wakati wa vita unaonekana kuwa na mguso maalumu. Hakuna
shaka kuwa, mikutano kama hiyo itasaidia kufungua njia za kukabiliana na
vitendo hivyo, pamoja na kuwazingatia waathirika wa vitendo vya ubakaji
kwenye maeneo ya vita. Kuwepo mikakati madhubuti na imara ya
kuwafuatilia kisheria watenda jinai hizo sanjari na kuwasaidia
waathirika wa vitendo hivyo, kutazuia kuongezeka na kukaririwa mara kwa
mara vitendo vya ubakaji kwenye maeneo ya vita.
No comments:
Post a Comment