Jenerali Fransisco Soriano Kamanda wa majeshi ya Ufaransa katika Jamhuri
ya Afrika ya Kati amesisitiza kwamba majeshi ya nchi hiyo yataanza
kuondoka nchini humo tarehe 15 Septemba mwaka huu. Majeshi ya Ufaransa
yalipelekwa Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Disemba mwaka jana baada ya
kushadidi mapigano Bangui, mji mkuu wa nchi hiyo ya Kiafrika. Rais
Francois Hollande wa Ufaransa alidai kuwa, operesheni hiyo ilifanyika
kwa lengo la kuisaidia serikali ya Bangui na kulinda maisha ya raia wa
nchi hiyo.
Hivi sasa nchi hiyo ya Magharibi imetangaza azma ya kuondoa
majeshi yake nchini humo, baada ya kuyapeleka huko miezi sita iliyopita.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Aprili mwaka huu, Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio jipya baada ya hali ya kibinadamu
kuwa mbaya nchini humo na hasa wimbi la mauaji yaliyofanywa na kundi la
wanamgambo wa Kikristo la Anti Balaka dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa azimio hilo, iwapo jamii ya kimataifa haitatoa radiamali
ya haraka kuhusiana na hali mbaya ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kuanzia
tarehe 15 Septemba mwaka huu, kitapelekwa mjini Bangui kikosi cha
wanajeshi wa kulinda amani wapatao elfu kumi na askari polisi elfu moja
mia nane. Ban Ki moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya
kutetea haki za binadamu mara kadhaa yametahadharisha juu ya uwezekano
wa kutokea janga la kibinadamu nchini humo. Umoja wa Mataifa mapema
mwaka huu uliunda kamati iliyokuwa na jukumu la kuchunguza kwa kina
chanzo cha mauaji, unyama na ukatili uliofanyika nchini humo. Uchunguzi
huo utaweza kuweka bayana iwapo kile kilichofanywa na wanamgambo wa
muungano wa Seleka na wale wa Kikristo wa Anti Balaka, ni jinai za
kivita na dhidi ya binadamu au la. Baraza la Usalama lilitahadharisha
kwamba mashambulio ya kulipiza kisasi kati ya Waislamu na Wakristo mjini
Bangui, ni mwanzo wa kuibuka vita vya pande zote, mauaji ya kimbari na
kikabila nchini humo. Naye Bwana Mull Sebujja Katende mwakilishi wa
Uganda ambapo nchi yake ni mwenyekiti wa mzunguko wa Baraza la Amani na
Usalama la Umoja wa Afrika amesisitiza kwamba moja ya vifungu vya
baraza hilo ni kutiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka wale wote
waliotenda jinai kwenye nchi mbalimbali za Kiafrika. Hivi sasa kuna
makubaliano kati ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika na
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya ulazima wa kufanyiwa
uchunguzi wa kina matukio yote ya mauaji yanayofanyika barani humo.
Pamoja na hayo yote, hatua ya Ufaransa ya kupeleka wanajeshi wake
wasiopungua 2,000 huko Jamhuri ya Afrika ya Kati haikuweza kusaidia
kurejesha amani na utulivu nchini humo, bali ilichangia kwa kiasi
kikubwa mwendelezo wa mauaji ya kundi la Anti Balaka dhidi ya
Waislamu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment