Jumuiya na taasisi mbalimbali za kimataifa zimetoa tahadhari
kubwa kuhusu hali mbaya ya wakazi wa eneo la Ukanda wa Ghaza huko
Palestina kufuatia kuanza kipindi cha majira ya joto katika pwani ya
Bahari ya Meditteranian.
Taarifa iliyotolewa na jumuiya zisizo za serikali za Palestina
imesema wakazi wa Ukanda wa Ghaza wanasumbuliwa na uhaba mkubwa wa maji
safi na bidhaa muhimu kama dawa na chakula, kutokana na siasa za
kidhalimu za utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kulizingira eneo
hilo. Jumuiya hizo zimesisitiza kuwa, mzingiro wa Israel unaoendelea kwa
miaka saba mfululizo katika eneo hilo ni sawa na kuwapa mateso ya umma
wakazi wote wa Ghaza na ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria
za kimataifa.
Hali mbaya ya watu wa Ghaza kutokana na siasa za kidhalimu na kigaidi
za Israel katika eneo hilo imefikia kiwango cha tahadhari na inaripoti
kuwa wagonjwa wanaolazwa katika hospitali na vituo vya afya ni mbaya
sana kutokana na joto kali na ukosefu wa dawa na zana za tiba.
Ukanda wa Ghaza wenye jamii ya watu zaidi ya milioni moja na nusu,
unazingirwa na utawala ghasibu wa Israel kwa miaka saba sasa na viongozi
wa utawala huo dhalimu wamekuwa wakizuia kuingizwa huko bidhaa na
mahitaji muhimu hususan dawa na zana za tiba.
Awali Wakala wa Misaada kwa Wapalestina wa Umoja wa Mataifa UNRWA
ulikuwa umetahadharisha juu ya hali mbaya ya wakazi wa Ghaza. Mkurugenzi
wa Operesheni za UNRWA Robert Turner ameitaka jamii ya kimataifa
kufanya jitihada kubwa za kukomesha mzingiro wa Ghaza.
Maafisa wa UNRWA wanasema eneo la Ukanda wa Ghaza linasumbuliwa na
uhaba mkubwa wa dawa na zana za tiba na kwamba akiba ya dawa katika eneo
hilo imemalizika.
Mbali ya hayo watu wa Ghaza wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji
safi na iwapo hali hiyo itaendelea watakumbwa na mgogoro mkubwa wa
ukosefu wa maji.
Mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa Ghaza umewafanya Wapalestina
milioni moja na nusu wakose huduma muhimu za kimsingi na kuwatumbukiza
wengi wao katika umaskini na ukosefu wa kazi.
Kwa sababu hiyo wafuatiliaji wa mambo wanasisitiza kuwa umewadia
wakati kwa walimwengu kukomesha kimya chao mbele ya jinai zinazoendelea
kufanywa na utawala haramu wa Israel katika eneo hilo la dunia na kupaza
sauti zao kukemea ukatili huo unaofanyika katika karne ya 21 tena kwa
msaada na hiyama ya nchi zinazodai zimestaarabika.
Ni kwa sababu hiyo pia ndiyo maana jumuiya mbalimbali za Kipalestina
na ile ya UNRWA zikamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
kukomesha haraka hali mbaya inayowasumbua wakazi wa Ukanda wa Ghaza.
No comments:
Post a Comment