![]() |
Rais Robert Mugabe |
Rais Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe amesema kuwa, anakusudia
kung'atuka madarakani lakini bila ya kuzingatia matakwa na mashinikizo
yanayotolewa na nchi za Magharibi. Kwenye mahojiano aliyofanyiwa na
gazeti la serikali la Herald la nchini humo, Rais Mugabe amesema kuwa,
sababu kuu ya kuendelea kubaki madarakani kwa zaidi ya miaka 30 sasa, ni
kukabiliana na njama za nchi za Magharibi za kutaka kubadilisha muundo
wa uongozi nchini humo.
Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 89, ameiongoza
Zimbabwe tokea ilipojipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza mwaka
1980. Rais wa Zimbabwe amesema kuwa, hatasalimu amri mbele ya
mashinikizo ya nchi za Magharibi ya kumtaka aondoke madarakani. Amesema,
ataondoka madarakani pindi atakapoona chama chake cha Zanu PF kina
umoja na mshikamano zaidi. Uchaguzi ujao wa rais nchini Zimbabwe
unatarajiwa kufanyika Agosti 14, na Mugabe atachuana vikali kwenye
uchaguzi huo na hasimu wake wa kisiasa Morgan Tsvangirai kutoka chama
cha MDC ambaye pia ni Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini
humo.
No comments:
Post a Comment