Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, June 9, 2013

Kujimwaya mwaya

Kwa muda wa miaka mingi Tido Mhando amekuwa akifanya kazi ya utangazaji, kazi ya mapenzi yake tangu utotoni. Kazi iliyomwezesha kufanya mengi, kuona mengi, kusafiri sana na hata kukutana na watu wengi wakiwamo wakuu na viongozi wa nchi mbalimbali duniani. Mengi ya haya ndiyo anayoendelea kuyaelezea kwenye makala zake hizi za kila Jumapili. Wiki iliyopita, Tido alisimulia jinsi siku yake ya kwanza ya kutangaza Radio Tanzania Dar es Salaam, (RTD) mwaka 1969, peke yake ilivyomfikia bila ya kutarajia, lakini akaifanikisha vyema na kuanzia hapo akawa ameanza kuaminika na kulijenga jina lake. Sasa endelea…
Naam, niliuvamia ulimwengu wa kutangaza redioni kwa nguvu na mbwembwe zote. Kwa muda wa miaka mingi nilikuwa nimejiandaa kusuburi nafasi hii. Nilipokuwa mtoto na hasa nilipokuwa shule nilikuwa napenda kuigiza mambo mbalimbali ya utangazaji kila nilipopata fursa.
Kuna nyakati darasani nilikuwa nawanyamazisha wenzangu na kuigiza nawasomea taarifa ya habari. Kuna saa kwenye viwanja vya michezo nilikuwa naigiza natangaza mpira na wakati mwingine bwenini nilikuwa nawachangamsha wenzangu kwa kujifanya DJ, nikicheza santuri za muziki kwa madoido yake. Hivyo fursa halisi iliponifikia, nilikuwa tayari sana kwa jukumu hilo.
Kwa hiyo nafasi yangu ya kwanza ikawa ni hiyo ya kuendesha vipindi vya muziki, jambo ambalo nililifurahia sana, hasa pale nilipokuwa nikipangwa zamu kwenye idhaa ya biashara niliyoanzia kutangaza siku yangu ya kwanza ya kujichana hewani nikiwa peke yangu.
Nilionyesha kipaji changu na umahiri mkubwa katika kuchangamka na muziki. Nikisifiwa kwa uchaguzi murua wa vibao vya kusisimua enzi hizo za wagosi wa kaya Jamhuri Jazz na “Shingo ya Upanga” au Atomic Jazz na ”Leo Nakupasulia” ama Kiko Kids wa Tabora au Polisi Jazz na wimbo wao wa “ Huko Magomeni”.
Au unisikie kwenye yale mapachanga ya kutoka “Zaire”, ya siku hizo sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), nilivyokuwa nikijimwaga na magoma ya Bavon Marie Marie au Verckys ama looh niwe nimeachia “Tambola ya Makili” ya Johnny Bokelo au “Mado” ya mwenyewe baba yao, Franco Lwambo Makiadi, utapoa.
Hata hivyo, kwa kuwa bado nilikuwa kijana mno basi maisha hayo ya ujana ujana nami yakawa yamenivaa nje na ndani ya kazi. Wakati huo ulikuwa ni enzi za muziki tukiuita wa “Soul” yaani Soul and Rhythm and Blues ambao ndiyo mwanzo wa hizi R&B za kisiku hizi na wenyewe tukijiita Masoul brothers na Masoul Sisters.
Hizi ndizo zilikuwa enzi za akina James Brown - “Say it loud I’m black and proud”, Wilson Picket - “In the midnight hour”, Aretha Franklin - “Respect”, Sam and Dave - “Hold on I’m coming”, Eddie Floyd – “Knock on wood”, Otis Redding na wengine wengi.
Hapa nyumbani zikawa enzi za muziki wa bugi ambapo vijana walikuwa wakicheza muziki wao hasa wakati wa mchana. Zikiwepo Bendi maalumu za vijana kama vile The Rifters na Adam Kingui pamoja na vijana wa pale magomeni wa The Fleming Stars.
Kwa hiyo mimi sikubaki nyuma kamwe kwenye minyumbuko hii, nikijimwaga vilivyo katika aina zote hizi za muziki. Nilikuwa nahakikisha ya kwamba nikiwa hewani kunakuwa na heka heka kweli kweli.
Nakumbuka siku moja nilikuwa zamu ya jioni kama kawaida mle studio mambo yakawa moto mtindo mmoja. Sishikiki hata kidogo, huku pamoja na biridi kali ya studio nilikuwa nimevua shati, kwani mwenyewe pia nilikuwa nikijimwaga kwa kucheza kwa nguvu.
Ghafla nikamwona dirishani mkurugenzi wangu, Mzee Martin Kiama akitaka kuingia mle studio, nikajua kapandisha na mambo yatakuwa moto maana hakuwa akipendelea mikeke ya aina ile niliyokuwa nikiendelea nayo. Hivyo nikawajibika kufikiri haraka haraka. Nikaamua kuwasha “microphone” na kwa hiyo taa za studio zikawaka, kuashiria ya kwamba mtu haruhusiwi kuingia ndani.
Mzee Kiama akasubiri kwa muda mfupi na baadaye akaondoka nami nikaendelea na majonjo yangu. Kumbe mambo hayakuishia hapo. Mapema asubuhi siku iliyofuata, mkurugenzi huyo akamwita Mkuu wa Idhaa hiyo ya Biashara, Ellie Mbotto, kunishtaki.
Mzee Kiama alisikika akimuuliza mkuu wa idhaa, “Huyu kijana kwani anavuta bangi”? Ellie Mbotto alimjibu kwa kumwambia wala havuti hata sigara. Mkurugenzi akaamuru nifungiwe kutotangaza kwa muda miezi mitatu.
Adhabu hii iliniuma kweli kweli maana tayari nilikuwa nimeanza kuwa maarufu. Kwa hiyo wasikilizaji walikuwa wameanza kuuliza kulikoni? Sasa kipindi hicho cha mfungo kilipomalizika nikarudi hewani kwa kishindo kingine.
Siku hiyo nikawaarifu mashabiki wangu ya kwamba wasiwe na shaka hata kidogo, nimerejea ulingoni na ni mzima kama chuma, nikitia vikorombwezo kwa kuwaambia kuwa mambo ndiyo sasa yatakuwa mazuri zaidi maana katika muda huo ambao nilikuwa nimepotea hewani nilikuwa mafunzoni.
Duu, kumbe wakati mimi nikibwabwajika hivyo hewani kwa mara nyingine Mzee Kiama alikuwa ananisikiliza. Safari hii akaamua kuniita mwenyewe siku ya pili yake. Akasema, umesema uwongo kwa wasikilizaji, kwa hiyo akaniongezea adhabu kwa muda mwezi mmoja zaidi.
Sasa sijui ulikuwa ni utundu wa ujana ama vipi maana hali hii ya kunifungia fungia iliendelea kiasi kwangu ingawaje nje wenzangu walikuwa wakiniona kwamba sikuwa mtukutu hivyo na wala sikuwa mtu wa fujo fujo hivyo.
Nakumbuka mara nyingine ilikuwa ni wakati wa mashindano kandanda ya kombe la Taifa Cup mwaka 1973. Mashindano haya ya kila mwaka yalikuwa maarufu sana wakati huo nchini yakiwa na ushindani mkubwa sana wa kimkoa.
Mikoa iliyokuwa ikitamba siku hizo ilikuwa Dar es Salaam, Morogoro, Kilimanjaro ambayo hasa ilikuwa ikiundwa na timu ya Shamba la Sukari la TPC, Tabora, Tanga na kiasi Mwanza. Mikoa hii ilipokuwa ikikutana ilikuwa ni patashika na nguo kuchanika. Nchi nzima siku hiyo ikazizima.
Tido Mhando - aliyekuwa mkurugezni wa TBC

Sasa mwaka 1972, Morogoro ndiyo waliibuka na ubingwa. Basi bendi maarufu za muziki mkoani humo zikatunga nyimbo kadhaa za kuisifu timu yao kwa kishindo.
Mechi ya nusu fainali mwaka uliofuatia 1973, Morogoro ikakutana na Tanga ya akina Abdallah Luo, Mwabuda, Omar na Saleh Zimbwe, Mahadhi, Kinanda, Kajembe na wengineo. Ngoma kali kweli kweli. Siku hiyo mimi nilikuwa ni mtangazaji wa zamu studio Idhaa ya Taifa. Mechi inachezwa Uwanja wa Karume, Ilala.
Mchezo ulipomalizika Morogoro wakajikuta wamelala kwa Tanga kwa kipigo cha mabao 3-1. Mimi nikawa narukaruka. Nikaenda maktaba nikakusanya nyimbo zote zile ambazo bendi za Morogoro waliziimba mwaka uliopita waliposhinda kuisifia timu yao.
Kwa hiyo mara tu kipyenga cha mwisho kilipopulizwa mimi nikawa nazicheza zile nyimbo huku nikiingilia kati na kwa masihara nikitangaza yale matokeo ya siku ile ya kipigo cha mabao 3-1.
Siku hizo Katibu Mkuu Wizara ya Habari alikuwa Daniel Mloka mwenyeji wa Morogoro. Kwa hiyo utani ule haukumfurahisha hata chembe. Mapema tu siku ya pili akaja Pugu Road, RTD, kachukia ile mbaya. Na yeye akanitangazia kiama kunifungia kwa miezi mingine mitatu. Kuanzia hapo nikawa nimekoma na hii mizaha mizaha.
Niliporejea hewani nikawa mtu wa nidhamu, lakini bado makeke sikuacha, huku nikitia mbwembwe kama kawaida yangu. Na ndipo siku moja asubuhi mjomba Salim Seif Nkamba akaniiita ofisi kwake.
Mjomba alikuwa kipande cha mtu. Amejengeka vilivyo. Enzi zake huko nyuma alikuwa mwana masumbwi mashuhuri sana akiwa amezipiga hadi kwenye kiwango cha ngumi za ridhaa za kimataifa. Wakati huo yeye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Ngumi cha Taifa. Vilevile mwamuzi wa ngumi wa kimataifa.
Sasa siku hiyo “mjomba”, kama alivyokuwa akifahamika zaidi aliniita kwa jambo jingine kabisa. Aliniiambia ya kwamba kampuni inayotenegenza Betri za tochi na redio ya “Eveready” ilikuwa imeamua kudhamini kipindi maalumu cha salamu za vijana na kwa hiyo mimi nimechaguliwa kukiendesha.
Nilitoka kwenye ofisi ile ya “mjomba” nikiwa nimefurahi kupindukia maana nilijua hii ndiyo nafasi niliyokuwa nikiisubiri ya kuwa na kipindi changu mwenyewe idhaa ya biashara. Kipindi chenyewe kilikuwa kinaitwa salamu za vijana na Matineja. Ukiwa ni ukumbi wa vijana wa kujimwaya mwaya kwa salamu na ule muziki wa upendao wa “Soul”.
Kilikuwa ni kipindi cha saa moja kila Jumapili usiku. Nikitakiwa zaidi kucheza zile nyimbo za soul za akina James Brown na wenzake. Kipindi kama hiki kilikuwa pia kinaendeshwa na Sauti ya Kenya (VOK siku hizo, sasa KBC), mtangazaji akiwa Leonard Mambo Mbotela.
Kabla ya kuanza rasmi nilifanya maandalizi. Nikaanza kufikiria jina zuri la kutumia. Hadi wakati huo nilikuwa nafahamika kama Dunstan Mhando, jina ambalo nililiona halina mvuto sana kwa utangazaji.
Katikati yake nilikuwa na jina la Theodore likitamkwa “Theado” ambalo ni jina la babu yangu aliyekuwa mwalimu enzi zake. Kwa hiyo nikawa natafuta jina la nguvu la utangazaji
Ndipo nilipokumbuka ya kwamba baba yangu, Mwalimu Daniel Mhando enzi hizo, alikuwa anapendelea zaidi kuniita jina la baba yake, hilo la Theodore akilikatisha kwa kuniita Tido. Aaah nikaona kwa kweli Tido Mhando wa salamu za mateneja litakuwa sawia kabisa.
Kwa hiyo mara tu nilipoanza kukiendesha kipindi hiki nikalitambulisha rasmi jina langu la “Tido Mhando” huku nikijipachika cheo cha “Senior Soul Brother” na huo ukawa mwanzo mpya kabisa kwangu kwa kupata umaarufu usio na mfano hasa kwa vijana wenzangu, kwani nadhani nilikuwa miongoni mwa waliokuwa vijana mashuhuri zaidi nchini wakati huo.
Nakumbuka siku moja nilikuwa kwenye gari la kazini tukampitia kwenye shule ya wasichana ya Kisutu kumpeleka mwenzetu aliyekuwa na miadi ya kikazi hapo. Tulipofika pale, wanafunzi wakapata habari kwamba nilikuwamo kwenye lile gari la Radio Tanzania.
Wakaja kulivamia gari lile karibu shule nzima, huku wakipiga kelele wakitaka nitoke. Mimi nikawa naona “aibu” nikawa nimejificha katikati ya wenzangu huku shangazi Thecla Gumbo ambaye alikuwamo, akiniambia “acha ujinga wewe” moyoni nilikuwa nikijisemea “angejua”.

No comments: