Dodoma. Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwasili mjini Dodoma,
ambapo pamoja na mambo mengine atakutana na Kamati ya Bunge ya Bajeti
ikiwa siku chache kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali
itakayoainisha Mapato na Matumizi yake kwa mwaka wa fedha 2013/14, Juni
13.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge imekuwa na vikao karibu kila siku, wakati
mwingine vikimalizika usiku ili ikijiweka sawa kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali.
Hata hivyo, habari zinadai kuwa ugumu uliopo ni
namna ya kupata fedha kwa asilimia 100 kwa ajili ya kutekeleza shughuli
mbalimbali za maendeleo na matumizi ya kawaida kwa wizara na Idara za
Serikali.
Chanzo chetu kilieleza kuwa pamoja na 'kukuna
kichwa' jinsi ya kupata fedha hizo, hata utekelezaji wa bajeti ya
2011/12 na 2012/13, ulikuwa mgumu kwa kuwa baadhi ya wizara na
taasisi zake zilipata nusu ya bajeti iliyopitishwa au asilimia 30 ya bajeti nzima.
Upatikanaji wa fedha hizo chini ya asilimia
unatarajiwa kwa wizara na taasisi zake huku ikielezwa kuwa ni kutokana
na kumegwa kwa asilimia za mafungu kulikosababishwa na kuongezeka kwa
matumizi ya Serikali zikiwemo dharura.
Chanzo kilipasha kuwa, wakati hali ikiwa hivyo,
hadi kufikia juzi kila Wizara ilishawasilisha taarifa zake mbele ya
kamati hiyo iliyokuwa ikikutana katika Ukumbi wa Pius Msekwa mjini
Dodoma, huku wizara nyingi mbali na kuwasilisha taarifa za mafungu yao
ya bajeti kwa mwaka 2013/14, zimeomba kuongezewa kasima kama kuna
uwezekano.
Itakumbukwa, wakati akiwasilisha bajeti ya mwaka
2012/13 Juni 14 mwaka jana, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema
kuwa bajeti hiyo imelenga kukabiliana na changamoto za uchumi ikiwa ni
pamoja na kuongeza fursa za kuuza, kushughulikia uhaba wa chakula nchini
na kupambana na mfumuko wa bei.
Alisema pia kuwa mpango wa Serikali ni kuendelea
kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kusimamia matumizi, kushughulikia
ukosefu wa ajira hasa kwa vijana na kuwekeza katika miundombinu ya
nishati ya umeme hasa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam.
Kingine alichokisema ni ujenzi wa barabara,
bandari na reli ya kati ili kupunguza gharama za kufanya biashara na
kuongeza tija katika uzalishaji; pamoja na kulipa madeni ya ndani na
nje.
Kutokana na hali hiyo, chanzo hicho kilisema kuwa ndiyo maana
juzi wakati Waziri wa Fedha, alipowasilisha hotuba ya makadirio ya
mapato na matumizi ya wizara yake, alisema mpango uliopo ni kubana
mianya ya ukwepaji kodi ili kuongeza pato la taifa.
Wakati akijibu hoja mbalimbali za Wabunge na
hotuba ya Kambi ya Upinzani juzi, Waziri Mgimwa alisema Serikali imeanza
kubana mianya yote ya ukwepaji kodi ikiwemo kufuta utaratibu wa
kuingiza mzigo moja kwa moja kutoka nje bila kukaguliwa.
Mgimwa alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
ilifanya ukaguzi wa makontena 520 bandarini kuanzia Aprili 8 hadi 31,
2013, na makontena 492 yalikuwa safi, lakini 188 yalikutwa na mizigo
inayokinzana na nyaraka.
"Kontena zilitozwa kodi na hii ni wazi kuwa
kulikuwa na mianya ya muda mrefu ya ukwepaji wa kodi kwa kipindi kirefu.
TRA wamefanya kazi na kupatikana kodi kwa makontena tofauti.
Kuhusu misamaha ya kodi kwa ajili ya kuongeza pato
la taifa, Waziri Mgimwa alisema kuwa kwa sasa wanakusanya Sh800 bilioni
kwa mwezi na kambi ya upinzani ilisema makusanyo yanaweza kufika Sh1
trilioni kama misamaha itaondoshwa.
Hata hivyo, Waziri Mgimwa alisema kuwa hana
Mamlaka ya kusamehe kodi na anachokifanya ni kuangalia misamaha ya kodi
kwa kuangalia sheria zilizoainishwa na Bunge.
Mgimwa aliwataka wabunge kutoa uamuzi wa aina gani
ya kodi ifutwe ndipo achukulie hatua. "Ninawaomba mseme wenyewe, ni
wapi panastahili kupunguza msamaha, sije nikafanya mambo kuwa juu ya
mamlaka yangu," alisema.
Habari kutoka ndani ya Kamati ya Bajeti inasema
kuwa mipango iliyopo katika mwelekeo wa bajeti ni kuhakikisha maeneo
yote yenye mianya ya ukwepaji kodi yanabanwa ili kuongeza Pato Ghafi la
Taifa, GDP.
No comments:
Post a Comment