Hii ni baada ya serikali kutangaza kusitisha utoaji mizigo bila kukaguliwa
katika bandari ya Dar es Salaam, wakwepa kodi wakubwa wamekejeli na
kusema “ni nguvu ya soda na ni upepo tu utapita” kwa maelezo kwamba
mtandao haujatetereka.
Habari kutoka kwa watu walio karibu na wafanyabiashara wanaotuhumiwa
kukwepa kodi, zinaeleza kwamba wameanza kuikejeli hatua ya serikali na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kudhibiti mizigo inayoingia nchini kwa
kudai kwamba hatua hiyo ni kupunguza kelele za watu waliowaita ‘wambea’.
“Wametuambia tusubiri muda si mrefu kazi ya kupitisha mizigo
itaendelea maana mtandao wao uko pale pale na wataanza tena kutupitishia
mizigo yetu kwa mtindo ule ule wa ‘direct release’.
“Tumewashitukia na sasa bora tupitie mkondo halali wa TRA badala ya
kutuingizia hasara,” alisema mfanyabiashara wa Kariakoo, ambaye
amejikuta akipata hasara baada ya mizigo yake kutozwa faini kubwa kwa
kudanganya aina ya mizigo baada ya kupitia kwa wafanyabiashara
waliobanwa sasa na TRA.
Baada ya gazeti hili kuandika mfululizo taarifa kuhusiana na ukwepaji
kodi unaotumia utaratibu wa ‘ditect release’, TRA ilisitisha ghafla
utaratibu huo na kuanza kufanya ukaguzi maalumu uliobaini ukwepaji
mkubwa wa kodi unaofanywa na wafanyabiashara wachache wanaodanganya aina
ya mizigo na hata thamani halisi.
Suala hilo likaibukia bungeni, siku chache baada ya Tanzania Daima
kuandika Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, alivyoshitukia ukwepaji
kodi huo.
Akihitimisha bajeti yake, Waziri Mgimwa, alisema serikali
imesimamisha utaratibu wa utoaji wa mizigo moja kwa moja bandarini na
kuanzia sasa mizigo yote itakaguliwa bila kujali nyaraka
zitakazoonyeshwa.
Alisema hatua hiyo imekuja baada ya kugundulika kwa ukwepaji wa kodi
kwa kutoa nyaraka tofauti na uhalisi wa mizigo iliyopo katika kontena
husika kunakofanywa na baadhi ya makampuni ya kutoa mizigo katika
bandari hiyo.
Alisema kutokana na udanganyifu huo, kuanzia sasa ukaguzi utafanyika
kwa kuangalia aina ya mizigo, nchi iliyotoka, muhusika wa mzigo, na
historia ya mtoaji wa mzigo bandarini.
Kama ilivyoandikwa na Tanzania Daima katika habari yake ya uchunguzi,
Waziri Mgimwa alisema kutokana na kugundulika kwa udanganyifu huo kati
ya makontena 522 yaliyokuwepo 498 yalikaguliwa upya.
Waziri huyo alisema kati ya makontena hayo yaliyokaguliwa upya,
ilibainika kuwa 188 yalikuwa na nyaraka zinazoonyesha mizigo tofauti na
iliyokuwemo ndani ya makontena hayo na kwamba serikali ilipata sh
bilioni 1.24.
Katika taarifa ya Waziri Mgimwa inayothibitisha taarifa
zilizochapishwa na gazeti hili, makontena yaliyobainika kufanya
udanganyifu, yalikutwa na mizigo ya ziada aina tofauti na mizigo
iliyojazwa katika karatasi, wajazaji wengine kudai wana mzigo mdogo
thamani halisi ya mzigo.
Ilibainika kwamba bidha zilizobainika katika makontena hayo ni pamoja
na CPU, vyandarua (kwa sababu havitozwi ushuru), monitor za kompyuta,
solar panel (vifaa vya uzalishaji wa umeme wa jua), aluminiam na nguo.
Alisema serikali imegundua kuwa kuna udanganyifu unatumia mtandao wa
nyaraka feki katika kuondoa mizigo bandarini kwa kushirikiana na
mawakala wa usafirishaji na uondoshaji mizigo bandarini ambao si
waaminifu.
Katika maelezo yake bungeni, Mgimwa alisema serikali imeweza kuinasa
baadhi ya mihuri ya mawakala wanaoshughulika na utoaji wa mizigo
bandarini ambayo ni bandia.
Mbali ya udanganyifu huo, Tanzania Daima imebaini pia kuwapo kwa
mbinu chafu za kuiibia serikali mapato kwa njia ya mtandao zilizokuwa
zikifanywa na baadhi ya wafanyabiashara wanaopitishia mizigo yao bandari
ya Dar es Salaam, kabla ya TRA kugundua na kufanya mabadiliko makubwa
katika mfumo wake wa mtandao unaotumika kuidhinishia mizigo.
Taarifa hizo zilizothibitishwa na maofisa waandamizi wa TRA,
zilieleza kwamba wafanyabiashara hao ambao wanatajwa sana katika sakata
la ukwepaji kodi, walifanikiwa kuingia katika mtandao wa TRA na kuwa
wanabadili alama maalumu zinazoonyesha mizigo inaruhusiwa kupita bila
kukaguliwa.
Tayari kumekua na taarifa za mmoja wa wafanyabiashara anayetajwa
kuhusika na ukwepaji kodi ameamua kukimbilia nje ya nchi kukwepa hatua
zinazoweza kuchukuliwa dhidi yake.
Mbali ya mfanyabiashara huyo kutajwa kukimbia, taarifa zinaeleza
kwamba kuna wafanyabiashara kadhaa wa maeneo mbalimbali nchini ambao
wamepata mshituko mkubwa baada ya kubaini kwamba walikuwa wanawatumia
wafanyabiashara hao kukwepa kodi huku wengine wakifilisika baada ya TRA
kufanya ukaguzi upya wa mizigo yao.
Kampuni inayotajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa inatajwa kuwa ni ile
maarufu kwa uuzaji wa bidhaa za nyumbani na wahusika wanaelezwa
kujisahau sana na kufanya hadharani kwa kutumia majina ya vigogo wa juu
serikalini.
Kwa takriban miaka mitatu iliyopita serikali kama njia ya kuondoa
mizigo bandarini mapema kwa kuepusha mrundikano na msongamano wa mizigo
bandarini, iliruhusu baadhi ya mizigo ya wateja wakubwa iwe inachukuliwa
bila kukaguliwa.
Kitendo hiki japo kilionekana kuwa na lengo nzuri, kilikosolewa na
wengi kwa kile kilichoonekana kingeweza kikatumiwa vibaya na baadhi ya
wateja wakubwa kwa kukwepa kulipa kodi stahiki.
No comments:
Post a Comment