Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, May 1, 2012

Wabuni mbinu ya kusafirisha mihadarati

WAFANYABIASHARA wa mihadarati aina ya mirungi wemegundua mbinu mpya ya kuisafirisha ikiwa na dawa mbalimbali za binadamu zilizopitwa na wakati kutoka Kenya kuja Tanzania kupitia mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Wafanyabiashara hao wa bidhaa hizo haramu, wanatumia madumu ya mafuta ya kula ya lita tano, kumi na ishirini kwa kuyatoboa chini na kuyaziba kwa moto utadhani kuwa ni mafuta ya kula.

Pia wanatumia chupa za chai baada ya kutoa yai la ndani, mabegi ya nguo na maboksi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Kamishna Msaidizi Robert Boaz alisema wafanyabiashara hao walikamatwa katika kizuizi cha Polisi eneo la Kirumi.
Walikamatwa kwa nyakati tofauti mwaka huu katika mabasi ya Kampuni ya Zakaria na
Batco ambayo yanafanya safari zake kutoka Sirari kwenda Mwanza.

Aliwataja wafanyabiashara waliokamatwa kuwa ni Faima Athmani (38) na Esther Daniel (33) wote wakazi wa Nyambiti jijini Mwanza wakiwa na kilo 93 za
mirungi, Emanuel Alex (20) akiwa na kilo 30, na Ngofilo Ngeleja (40) akiwa na kilo 14.

“Wote hawa walikamatwa kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema ambao wamechoshwa na tabia mbaya za baadhi ya watu wanaokusudia kuharibu amani nchini kwa kuuza dawa za kulevya,” alisema.

Kamanda Boaz alisema kuwa dawa mbalimbali za binadamu zilikamatwa lakini hakuna mtu yeyote aliyejitokeza kuwa alikuwa anahusika nazo
hivyo jeshi hilo likazichukua na kuzifikisha kituoni kwa ajili ya hatua zaidi.

Dawa zilizokamatwa ni pamoja na Alu, Amoxiline, Qunin Syrup, Sp, dawa za usingizi na dawa za kifua kikuu ambazo tayari zimepitwa na wakati.

Aliwaomba wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa Polisi ili kufanikisha vita ya kuzuia uingizaji wa dawa za kulevya pamoja na za binadamu zilizopitwa na wakati.

“Tunawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwa watu wanaoathirika ni sisi wenyewe hivyo wakatae hali hii kwani polisi pekee hawawezi bila ushirikiano wao,” alisema Boaz.

Mirungi hiyo na dawa hizo zilikuwa zimetokea nchi ya jirani ya Kenya ambazo zilipita katika mpaka wa Sirari na kuingia nchini.
 

No comments: