Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Thursday, May 24, 2012

Kusailiwa makamanda wa kijeshi Kongo


Majenerali na makamanda wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hivi karibuni wataitwa kusailiwa juu ya uwezo wa kusimamia wanajeshi na kulinda wananchi wa eneo la mashariki mwa nchi hiyo. Jeshi la Kongo ambalo limeundwa kutokana na makundi tofauti ya waasi wa zamani, linakabiliwa na tuhuma mbalimbali za kukiuka haki za binadamu na kutenda jinai dhidi ya raia. Taasisi za kutetea haki za binadamu zinawatuhumu askari wa jeshi la Kongo kuwa wanafanya ubakaji, mauaji na wizi dhidi ya wakaazi wa mashariki mwa nchi hiyo. Wakimbizi wa Kikongo ambao wamekimbilia katika nchi jirani kama vile Rwanda wanasema kuwa, miongoni mwa masuala yanayowafanya wanajeshi wa Kongo wawadhuru raia ni ukosefu wa nidhamu na kucheleweshwa mishahara yao. Wakimbizi wa nchi hiyo ambao wamekimbia mapigano kati ya jeshi na waasi wa mashariki mwa Kongo, wanalalamika kwamba askari jeshi pia wanaamiliana nao vibaya kama vile wanavyofanyiwa na waasi.
Jeshi la Kongo kwa mara ya kwanza lilifanyiwa marekebisho baada ya kumalizika vita vya ndani nchini humo vya mwaka 1998 hadi 2003 na lina jumla ya askari 150,000 hadi 160,000. Hii si mara ya kwanza kwa askari wa jeshi la Kongo walioko katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kutuhumiwa kuwa wanahujumu, kupora na kuua raia. Ijapokuwa vita vya ndani vya Kongo vilimalizika rasmi miaka 10 iliyopita lakini mikoa ya Kivu kaskazini na Kivu Kusini bado inashuhudia machafuko. Shughuli za waasi wa Rwanda wa FDLR na waasi wa LRA wa Uganda, zinahesabiwa kuwa sababu kuu ya kuendelea machafuko huko mashariki mwa Kongo. Licha ya makundi ya waasi kupokonywa silaha baada ya kumalizika vita, lakini bado silaha zinapatikana kwa wingi katika nchi hiyo. Taarifa ya taasisi za haki za binadamu inaonyesha kuwa, kati ya mwezi Agosti hadi Novemba mwaka 2006,wanajeshi walitenda jinai kama vile kuua, kupora na kuwakandamiza wananchi wa maeneo ya mpakani mwa Kongo. Ripoti pia zinaonyesha kwamba matukio kama hayo yalikaririwa katika miezi ya Aprili hadi Agosti mwaka 2007. Kugunduliwa kaburi la umati lililokuwa na wahanga 40 katika mkoa wa Ituri ni ushahidi mzuri wa madai hayo. Ijapokuwa waasi wa zamani wa Kongo baada ya kufikia makubaliano ya amani na serikali ya Kinshasa mwaka 2009 walijiunga na jeshi la taifa, lakini bado askari wanaasi jeshi mara kwa mara. Mfano wa hivi karibuni zaidi wa suala hilo ni kikosi cha askari waasi wanaoongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda. Jenerali huyo ambaye hivi sasa amegeuka kuwa kiongozi wa kundi linalojiita Waasi wa Kongresi ya Taifa kwa ajili ya Kulinda Wananchi, anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kama ilivyokuwa kwa jenerali muasi Laurent Nkunda, na akikamatwa atahukumiwa katika mahakama hiyo. Wataalamu wa mambo wanasema, umbali mkubwa uliopo kati ya mji mkuu wa Kongo, Kinshasa na eneo la mashariki mwa nchi hiyo ni miongoni mwa masuala yanayopelekea serikali kushindwa kusimamia wanajeshi walioko katika mikoa ya Kivu. Pengine pia hali ya kijiografia ya Jamhuri ya Kidemokarasia ya Kongo ambayo inapakana na nchi 9 za eneo la Maziwa Makuu ya Afrika, imepelekea kuwepo mazingira yanayochangia kutokea mara kwa mara machafuko na migogoro ya kikabila katika maeneo ya mpakani.

No comments: