Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Wednesday, May 21, 2014

"Waganda wachukulie kwa uzito indhari za ugaidi"

Mkuu wa jeshi la Uganda, Jenerali Katumba Wamala amewataka raia wa nchi hiyo kuchukulia kwa uzito indhari zinazotolewa na polisi mara kwa mara kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi. Jenerali Wamala amekumbusha kwamba, wanamgambo wa al-Shabab bado wanaiangalia Uganda kwa jicho la hasira kutokana na nchi hiyo kuwa na wanajeshi nchini Somalia. Amesema polisi wanapotoa tahadhari huwa wamefanya uchunguzi na kupata taarifa za kuaminika za kiintelijensia na kwa mantiki hiyo haifai wananchi kupuuza tahadhari hizo.

Polisi ya Uganda imetangaza kuongeza maafisa wa usalama wanaopiga doria mjini Kampala ili kuepusha uwezekano wa nchi kushambuliwa na magaidi. Polisi ya nchi hiyo pia imetangaza ratiba maalum ya doria wakati wa mashindano ya kombe la dunia katika mchezo wa soka yanayotarajiwa kuanza baadaye mwezi ujao nchini Brazil. Itakumbukwa kuwa, mwaka 2010 wanamgambo wa al-Shabab walishambulia kwa mabomu kumbi kadhaa za starehe mjini Kampala wakati wa mechi ya fainali ya kombe la dunia ambapo zaidi ya watu 70 waliuawa.

No comments: