Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Friday, May 11, 2012

Mashambulio ya kigaidi nchini Syria na kuuawa raia wasio na hatia

Miripuko ya mashambulio ya kigaidi yaliyofanywa katika mji mkuu wa Syria, Damascus imepelekea kuuawa na kujeruhiwa mamia ya watu. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria imetoa taarifa ya kulaani mashambulio hayo ya kigaidi na kueleza kwamba jana asubuhi watu wasiopungua 70 waliuawa na wengine 400 walijeruhiwa kutokana na miripuko iliyosababishwa na mabomu yaliyokuwa yametegwa ndani ya magari mawili katika eneo lenye msongamano wa watu la Al Qazaz huko kusini mwa Damascus. Kwa mujibu wa taarifa hiyo viwiliwili 15 vya wahanga wa mashambulio hayo mawili ya kigaidi bado havijaweza kutambulika hadi sasa. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria imeongeza katika taarifa yake hiyo kuwa wengi wa majeruhi wa miripuko hiyo ni raia wa kawaida, na mbali na maafa ya roho za watu mashambulio hayo ya kigaidi yamesababisha pia hasara kubwa kwa mali za raia na za serikali.
Miripuko ya jana asubuhi mjini Damascus imetokea wakati makumi ya waangalizi wa kimataifa wakiwa nchini humo kusimamia usitishaji mapigano. Kwa mujibu wa mpango wa vipengele sita uliopendekezwa na Kofi Annan, mwakilishi wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika masuala ya Syria, usitishaji mapigano ulipaswa kuanza kutekelezwa tangu tarehe 12 ya mwezi uliopita wa Aprili, lakini waasi wanaobeba silaha wanaosaidiwa na baadhi ya nchi za Magharibi na za Kiarabu waliamua kuitumia vibaya hatua ya jeshi la Syria ya kuwaondoa askari wake katika baadhi ya miji na kuendeleza mashambulio yao ya kigaidi. Wakati waangalizi wa Umoja wa Mataifa wa kusimamia usitishaji vita wamefanya safari ya kuelekea huko Syria, Suzan Rice, balozi wa Marekani katika umoja huo amesema Washington ingali inaendelea kutoa mashinikizo kwa Syria ili kumng'oa madarakani Rais Bashar al Assad wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa televisheni ya Syria, masaa kadhaa baada ya kutokea miripuko, ujumbe wa wasimamizi wa Umoja wa Mataifa ulifika katika eneo la miripuko hiyo. Jenerali Robert Mood, kamanda wa wasimamizi hao wa Umoja wa Mataifa ambaye yeye mwenyewe alilengwa na mashambulio hayo ya kigaidi ya waasi wanaobeba silaha nchini Syria alisema baada ya kutembelea eneo la miripuko kwamba watu waliofanya mashambulio hayo wajue kuwa hatua na vitendo vya aina hiyo havitowezesha kupatikana ufumbuzi halisi wa mgogoro wa nchi hiyo. Mashambulio ya kigaidi ya hapo jana yamefanywa katika hali ambayo katika kuendeleza mchakato wa mageuzi ya kisiasa, serikali ya Rais Bashar al Assad imeendesha kwa mafanikio zoezi la uchaguzi wa bunge nchini kote kutokana na wananchi wengi kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo. Miripuko ya jana imeonesha kuwa waasi nchini Syria wameamua kufanya mashambulio hayo ya kigaidi ili kuyatia doa mafanikio hayo. Kwa miezi kadhaa sasa makundi ya kigaidi yanayopewa misaada na uungaji mkono na madola ya kigeni yameigeuza baadhi ya miji ya Syria kuwa uwanja wa machafuko na umwagaji damu, lengo lao likiwa ni kutaka kuonesha kwamba serikali ya Damascus ndio inayohusika na machafuko hayo ili kuandaa mazingira ya uingiliaji wa madola ya kigeni nchini humo

No comments: