Takriban watu 118 wameuawa kwenye
milipuko miwili ya mabomu katika mji wa Jos ulioko katikati mwa Nigeria.
Habari zinasema milipuko hiyo imetokea kwenye kituo kimoja cha mabasi
mjini hapo jana Jumanne. Mratibu wa Ofisi ya Kitaifa ya Misaada ya
Dharura, Mohammed Abdulsalam amesema idadi ya vifo inaweza kuongezeka
kwani inaaminika kuna watu wengi waliofunikwa chini ya vifusi baada ya
magari kuanguka na baadhi ya majengo kuporomoka kutokana na kishindo cha
milipuko hiyo.
Hadi sasa hakuna mtu au kundi lililodai kuhusika na
shambulizi hilo lakini baadhi ya watu wanalinyooshea kidole cha lawama
kundi la Boko Haram ambalo katika siku za huko nyuma limewahi kukiri
kutekeleza mashambulizi ya aina hiyo.
Rais Goodluck Jonathan ametoa taarifa ya
kulaani mashambulizi ya hapo jana na kuyataja kuwa ya kinyama na ya
kishetani. Amesema serikali haitapigishwa magoti na magaidi na kwamba
kila juhudi zitafanywa ili kuwakamata wahusika.







No comments:
Post a Comment