Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Saturday, May 5, 2012

Wananchi wa Iran washiriki kwa wingi katika duru ya pili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu

Kwa mara nyingine tena wananchi wa Iran wamejitokeza na kushiriki kwa wingi katika duru ya pili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu au kwa jina jingine bunge, ambao umefanyika jana Ijumaa. Mafisa wanaosimamia uchaguzi huo wamesema kuwa idadi ya wananchi walioshiriki katika duru hii ya pili ya uchaguzi wa bunge la awamu ya tisa imekuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na idadi ya watu walioshiriki katika duru ya pili ya uchaguzi uliopita.
Akizungumza mara tu baada ya kupiga kura katika dakika za mwanzo za kufunguliwa vituo vya kupigia kura kote nchini, Ayatullahil Udhma Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amewataka wananchi kushiriki kwa wingi, kama ilivyo kawaida yao, katika duru hii ya uchaguzi kwa sababu jambo hilo litawapa wabunge wanaochaguliwa itibari na uwezo zaidi wa kutekeleza majukumu yao bungeni kwa maslahi ya taifa.
Skeikh Hashimi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran pia ameshiriki mapema katika uchaguzi huo na kusema kuwa kushiriki kwa wingi wananchi kwenye uchaguzi huu kutawasaidia viongozi wa mfumo wa Kiislamu kutekeleza vizuri kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni ya kuimarisha harakati za uzalishaji wa taifa na kuunga mkono kazi pamoja na uwekezaji wa Kiirani.
Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushari ya Kiislamu pia akizungumza mara tu baada ya kukagua namna uchaguzi ulivyokuwa ukifanyika katika mitaa ya kusini mwa jiji la Tehran amesema mahudhurio ya wananchi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge yalikuwa ya kuvutia sana na kuongeza kuwa mahudhurio kama hayo katika duru hii ya pili ya uchaguzi yanaweza kuwa na nafasi muhimu katika kudhamini na kulinda haki za taifa la Iran.
Akizungumzia umuhimu wa uchaguzi wa leo, Ayatullah Ahmad Khatami, hatibu wa muda wa Swala ya Ijumaa ya mjini Tehran amesema kwamba utungaji na usimamiaji sheria ni moja ya nyadhifa muhimu za wabunge na kuwataka wasimame imara na kuzingatia uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao. Ramin Mehmanparast, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi wa jana kuna umuhimu mkubwa katika utekekelezaji wa siasa za nje na hasa katika kipindi hiki cha kukaribia kufanyika mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1 huko mjini Baghdad Iraq. Amesema kushiriki huko bila shaka kutawapa maafisa wa wizara iliyotajwa nguvu zaidi ya kufuatilia malengo na maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu katika ngazi za kimataifa. Amesisitiza kwamba vitisho vya maadui dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran vitapungua kwa kiwango kikubwa kwa kuzingatia wingi wa wananchi wanaoshiriki katika uchaguzi kwa lengo la kuunga mkono mfumo wa Kiislamu wa Iran.
Waandishi habari wa nje 274 wa kigeni na 850 wa ndani wameakisi habari zinazohusiana na uchaguzi huu. Duru ya kwanza ya uchaguzi huu wa bunge la Iran ambalo lina viti 290, ilifanyika tarehe Pili mwezi Machi uliopita.

No comments: