Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Wednesday, May 9, 2012

Kuchaguliwa rais mpya wa Ufaransa na athari zake kwa uhusiano na nchi za Afrika

Sisitizo lililotolewa na Rais mteule wa Ufaransa Francois Hollande la kuangalia upya uhusiano wa nchi hiyo na nchi za Kiafrika limepokelewa na kuwavutia wananchi wa bara hilo. Hollande amesema kwamba uhusiano baridi uliopo kati ya Paris na bara la Afrika ni wa kawaida kutokana na utendaji wa serikali za huko nyuma. Aidha amesema, uhusiano wa Paris na baadhi ya makoloni yake ya zamani katika kipindi cha huko nyuma ni wa kustaajabisha, na kudai kwamba atachukua hatua za kuuboresha. Hollande amesema, katika hatua ya kwanza atazingatia mshikamano wa kisiasa na kiuchumi na bara la Afrika na kisha kuzingatia lugha katika hatua ya pili. Rais huyo mteule wa Ufaransa amesisitiza kufanywa mabadiliko katika siasa za nje za nchi hiyo katika hali ambayo, wananchi wengi wa Afrika bado hawajasahau majeraha waliyosababishiwa na ukoloni wa Ufaransa barani humo.
Miongoni mwa masuala yanayofanya serikali ya Paris ichukiwe barani humo ni nafasi iliyokuwa nayo nchi hiyo katika mauaji ya kimbari ya Rwanda. Viongozi wa Rwanda wanasema kuwa, Paris iliusaidia utawala wa zamani wa nchi hiyo wa Wahutu, kuwaua kwa umati Watutsi 800,000 katika mauaji ya kimbari ya nchi hiyo ya Kiafrika. Tume Huru ya Kitaifa ya Rwanda ambayo iliundwa na serikali ya Kigali na kupewa jukumu la kukusanya ushahidi na nyaraka kuhusiana na mauaji hayo ya kimbari ya mwaka 1994, nayo pia ilitoa ripoti na kutangaza kwamba uongozi wa ngazi za juu wa kisiasa, kidiplomasia na kijeshi wa Ufaransa ulishiriki katika mauaji hayo. Kwa mujibu wa tume hiyo, Ufaransa iliwapatia mafunzo, silaha na suhula za kijeshi askari na wanamgambo wa Kihutu, na pia kushirikiana nao kisiri katika mauaji ya kimbari, kutesa na kubaka raia wa Rwanda. Katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa Ufaransa wamejaribu sana kulinda maslahi ya nchi hiyo barani Afrika, kwa kupunguza taathira hasi za uingiliaji wao katika masuala ya bara hilo. Safari za mara kwa mara za viongozi wa Ufaransa katika nchi za Afrika na kutoa mialiko kwa viongozi wa Kiafrika kuitembelea nchi hiyo kunadhihirisha wazi hamu ya Paris ya kuhuisha tena uhusiano na makoloni yake ya zamani barani humo. Wakati huo huo, Rais Nicolas Sarkozy aliyeshindwa katika uchaguzi wa hivi karibuni, alijaribu kuendeleza siasa za nje za nchi hiyo kwa nguvu zaidi, alipojitahidi kurekebisha taswira ya Paris katika fikra za Waafrika kwa kutumia kisingizio cha kulinda demokrasia na kulinda haki za binadamu. Uingiliaji wa Ufaransa nchini Ivory Coast na kuongoza katika kushawishi fikra za waliowengi duniani dhidi ya dikteta wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi, ni mifano inayodhihirisha jitihada za viongozi wa zamani wa Ufaransa za kuboresha sura yao katika bara hilo. Hata hivyo inaonekana kuwa sababu kuu ya uingiliaji wa Paris barani Afrika ni kupora utajiri wa bara hilo na kuokoa uchumi unaokabiliwa na migogoro wa nchi hiyo ya Magharibi. Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba, kuna tofauti kubwa kati ya mitazamo ya Sarkozy na Hollande kuhusu sera muhimu za Ufaransa. Katika hali ambayo Sarkozy alizichukulia nchi za Afrika kama milki yake na kuonyesha kiburi kuhusiana na bara hilo, Hollande kidhahiri ameonyesha kuwa na mtazamo wa wastani kuhusiana na bara hilo. Hata hivyo weledi wa mambo wanaamini kuwa, licha ya kuwepo tofauti hizo kati viongozi hao, lakini hakutakuwepo na mabadiliko makubwa katika kisiasa za Ufaransa mkabala na bara la Afrika katika kipindi cha urais wa Francois Hollande.

No comments: