Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Wednesday, May 9, 2012

Iran mwenyeji wa kikao kijacho cha Jumuiya ya NAM

Kikao cha 17 cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM kinafanyika leo na kesho huko Sharm Sheikh nchini Misri. Kikao hicho kinafanyika katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu Iran inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa NAM na kwa msingi huo inatarajiwa kuchukua rasmi uwenyekiti wa kiduru wa jumuiya hiyo. Kwa msingi huo maazimio ya kikao cha Sharm Sheikh yanatarajiwa kuwa agenda ya kikao kijacho nchini Iran. Ali Akbar Salehi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yuko Sharm Sheikh kushiriki kikao hicho cha NAM. Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni na wawakilishi wa nchi 120 wanachama wa NAM, wawakilishi wa nchi nyingine 28 , asasi za kimataifa ambazo ni wanachama watazamaji pamoja na nchi na asasi zisizo wanachama na vile vile shakhsia wa kisiasa na kimataifa akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa kiduru wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wanashiriki katika kikao cha NAM huko Sharm Sheikh.
Kikao cha Sharm Sheikh kinatarajiwa kujadili masuala mengi ya kieneo na kimataifa katika uga wa kisiasa, kiuchumi katika fremu ya matukio yanayojiri hivi sasa ulimwenguni na masuala yanayozihusu nchi hizo. Aidha suala la ustawi na haki za bianadamu ni miongoini mwa ajenda za mkutano wa leo na kesho huko Sharm Sheikh. Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM ni asasi ya kimataifa ambayo ina nchi wanachama 120 kutoka Afrika, Asia na Amerika ya Latini. Kimsingi NAM ni natija ya juhudi za kisiasa za miaka ya 50 zilizofanywa na nchi kama Cuba, Yogoslavia ya Zamani, India, Misri na Indonesia kwa lengo la kuanzisha kundi lenye mitazamo ya pamoja kuhusiana na masuala ya kieneo na kimataifa. Moja ya malengo ya Jumuiya ya NAM ni kupambana na ubeberu, ubaguzi na uvamizi. Kuishi kwa pamoja kwa amani, kuunga mkono haki ya nchi kujiainishia mustakbali wake, mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi wa nchi ni miongoni mwa malengo mengine ya kuasisiwa Jumuiya ya NAM. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, hivi sasa nchi wanachama wa NAM zimeingia katika duru mpya ya matukio yanayojiri ulimwenguni ambapo kigezo chake kikuu ni harakati ya mwamko wa Kiislamu kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati kwa upande mmoja na matukio yaliyosababishwa na matatizo ya kiuchumi katika ulimwengu wa Magharibi kwa upande wa pili. Matukio yaliyotokea Tunisia, Misri, Libya na Yemen na kupelekea kuondolewa madarakani viongozi wa nchi hizo yamepelekea kubadilika mahesabu na hali ya mambo katika eneo huku hali katika nchi za Bahrain na Saudia ikiingia katika hatua na marhala mpya. Katika hali ya hivi sasa pia Iraq imeingia katika hatua nyeti baada ya vikosi vya Marekani kuondoka nchini humo. Kwa muktadha huo, kuna haja ya kuongezwa ushirikiano wa kieneo kwa lengo la kutatua matatizo yaliyopo katika fremu ya uwezo wa NAM. Hata hivyo, hakuna shaka kuwa, jambo hilo linahitajia ushirikiano mkubwa ndani ya jumuiya hiyo muhimu ambayo katika kipindi chote cha uhai wake imekuwa ikibadilika kutokana na sababu za ndani na nje.

No comments: