Leo ni Jumamosi tarehe 20 Shaaban mwaka 1434 Hijria sawa na tarehe 29 Juni mwaka 2013.
Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita Vita vya Pili vya Balkan
vilianza baina ya Bulgaria na mjumuiko wa nchi za Serbia, Montenegro,
Romania, Ugiriki na utawala wa Othmania. Yapata mwaka mmoja kabla katika
Vita vya Kwanza vya Balkan, Bulgaria, Serbia, Ugiriki na Montenegro
zilizokuwa ni sehemu ya utawala wa Othmania, zilianzisha uasi dhidi ya
ufalme huo, na kutokana na kudhoofika utawala huo nchi hizo zilifanikiwa
kupata uhuru. Kwa utaratibu huo karibu asilimia 80 ya ardhi zilizokuwa
chini ya utawala wa Othmania barani Ulaya ikawa imeondoka katika
udhibiti wa utawala huo.
Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, iliyopita Visiwa vya
Ushelisheli vilivyoko katika bara la Afrika vilipata uhuru na wananchi
wa visiwa hivyo huiadhimisha siku hii ya tarehe 29 Juni kwa anuani ya
Siku ya Uhuru. Hadi katikati mwa karne ya 18 ambapo Wareno walikuwa
wamefanikiwa kuidhibiti ardhi ya Ushelisheli, visiwa vingi vya eneo hilo
vilikuwa havijagunduliwa na hakukuwa na mtu aliyekuwa akiishi katika
visiwa hivyo. Ni katika kipindi hicho, ambapo upenyaji wa Ufaransa
ulipoanza. Mwishoni mwa karne ya 18 wakati harakati za mapinduzi ya
Ufaransa zimepamba moto, majeshi ya Uingereza yaliyokuwa katika moja ya
maeneo ya Afrika yalivikalia kwa mabavu visiwa vya Ushelisheli.
Na siku kama ya leo miaka 1049 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya
Hijria, Ibn Nadim mwanahistoria na mtaalamu wa masuala ya vitabu wa
Kiislamu alifariki dunia. Umashuhuri wa mtafiti huyo unatokana zaidi na
kitabu chake maarufu cha faharasa. Katika kitabu hicho Ibn Nadim
amezitaja takriban elimu zote mashuhuri katika ustaarabu wa Kiislamu na
kisha kufafanua maisha na historia ya wanazuoni maarufu katika elimu
hizo. Kadhalika Ibn Nadim amevitaja humo vitabu na makala zilizoandikwa
kuhusiana na elimu hizo.
No comments:
Post a Comment