skip to main |
skip to sidebar
Chadema yagoma kutoa Polisi
Wabunge
wanne wa Chadema, Said Arfi (Mpanda Mjini), Tundu Lissu (Singida
Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti Maalumu)
wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na mkusanyiko usio halali kwenye
Uwanja wa Soweto jana.
Mkuu
wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jana kwamba
pamoja na wabunge hao pia wamewakamata watu wapatao 60 kutokana na
vurugu zilizozuka jana baada ya Polisi kuwatawanya kwenye uwanja huo
waliokuwa wamekusanyika kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi,
Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki kwenye mlipuko wa bomu uliotokea
kwenye uwanja huohuo, Jumamosi iliyopita.
Mbali ya viongozi hao, alisema wanawasaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
“Tunawasaka
wabunge ili tuwajumuishe na watu hawa kwa kosa la kuhusika na
mkusanyiko usiokuwa halali. Hadi sasa tumefanikiwa kulinasa gari la
Mbowe,” alisema Chagonja.
Pia
kamatakamata hiyo imemkumba Mpigapicha wa Kituo cha Televisheni cha
Channel Ten, Ashraf Bakari. Polisi walilazimika kutumia nguvu
kuwatawanya waombolezaji hao.
Awali,
Kamishna Chagonja alisema jana asubuhi kuwa wamelazimika kuzuia viwanja
hivyo kutumika baada ya wamiliki wake, AICC kuzuia shughuli za Chadema
kwenye eneo lao na kwamba upelelezi bado unaendelea katika viwanja hivyo.
Kamishna
Chagonja aliwaonyesha waandishi wa habari barua aliyosema imeandikwa na
uongozi wa AICC kuzua Chadema kuendelea kuutumia Uwanja wa Soweto.
Mabomu yarindima
Dalili
za kuzuka kwa vurugu zilianza kuonekana asubuhi baada ya polisi
kuzingira uwanja huo na kuzuia watu waliokuwa wameanza kufurika katika
eneo hilo kuanzia saa moja kuingia kwa ajili ya maombolezo.
Wakati Polisi wakiwa uwanjani, wananchi walijaa nje ya uwanja na kuonekana kama wamewazingira.
Viongozi
wa Chadema wakiongozwa na Mbowe waliwasili uwanja hapo yapata saa nane
mchana na kukuta zuio hilo na kuanza kuzungumza na wananchi ingawa FFU
walikuwa wakiwataka watu kutawanyika. Mabomu yalianza kurindima wakati
Arfi aliposimama na kuwahimiza wananchi kuelekea Hospitali ya Mount Meru
kwa ajili ya kuaga miili ya marehemu.
“Tuna
muda mfupi sana wa kuzungumza hapa, tunaomba wote tuelekee Hospitali ya
Mount Meru kuaga miili ya marehemu kwa sababu uwanja huu umezuiwa na
polisi,” alisema Arfi kabla ya kukatishwa na milipuko ya mabomu.
Awali,
Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema alitoa msimamo wa chama
hicho kuwa Mwenyekiti wao, Mbowe na Lema hawatatoa ushahidi wa tukio la
bomu wala kujisalimisha polisi kwa sababu hawana imani na jeshi hilo.
“Namtaka
Chagonja atangulie mahakamani, tutakutana hukohuko. Mbowe na Lema
hawatatoa ushahidi wala kujisalimisha polisi...
” alisema Lissu na
kuongeza:

“Kisheria haiwezekani polisi ambao ndiyo watuhumiwa ndiyo wadai kukabidhiwa ushahidi ili wauharibu.”
Mapema
Kamishna Chagonja aliwataka Mbowe na Lema kutoa ushahidi wa polisi
kuhusika na tukio la kurusha bomu kwenye mkutano wa Chadema la sivyo
polisi watatumia sheria kuwalazimisha kufanya hivyo.
Hekaheka
Baada
ya polisi kuanza kutupa mabomu saa 8.45 mchana, wabunge, viongozi
waandamizi wa Chadema na watu waliokuwa wamekusanyika walilazimika
kutimua mbio.
Watu
walioshuhudia tukio lile wanasema viongozi hao akiwamo Mbowe na
mwenzake Lissu walikimbilia kwenye magari yao. Lema alilazimika
kukimbilia kwa wachoma nyama ya nguruwe, (kitimoto) kwenye maeneo ya
Kaloleni.
Kabla ya polisi kurusha bomu mahali alipokuwapo Lema, mbunge huyo alisikika akisema:
“Jaribuni
kuvumilia, tunajaribu kuwasiliana Serikali ya Mkoa, ili watupe kibali
cha kuleta miili ya wapendwa wetu hapa, kuweni wastaarabu kwa sababu
mbele yetu kuna wana usalama ambao wanalinda amani, ingawa kufa ni kufa
tu, wenzetu wameshakufa na sisi ipo siku tutakufa, lakini kila
anayetangulia lazima tumzike kwa heshima zote.”
Kauli
hiyo iliwachefua polisi ambao walishatangaza amri ya watu kutawanyika
katika viwanja hivyo na kwamba hakutakuwa na suala la kuaga miili ya
watu hao katika eneo hilo. Ghasia hizo zilisababisha kusimama kwa
shughuli za biashara na kijamii kwa muda jijini Arusha huku watu
waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na maeneo yalikorushwa mabomu
wakilazimika kutoka nje kupata hewa safi baada ya nyumba hizo kujaa hewa
ya mabomu.
Polisi
waliokuwa wakirusha mabomu waliwakimbiza wananchi hadi maeneo ya Sakina
huku wakiendelea kufyatua mabomu kila walipoona mkusanyiko wa watu.
Katika
eneo la Kaloleni
, mkabala na Ofisi ya Mtendaji wa Kata hiyo baadhi ya
wafuasi wa Chadema walichoma matairi barabarani na kusababisha ifungwe.
Pia walichoma matairi katika eneo la Mianzini
Katika
eneo la Tanki la Maji
, Barabara ya kwenda Moshi, baadhi ya wafuasi wa
Chadema walipanga mawe barabarani na kusababisha msongamano wa magari.
Katikati ya jijini Arusha barabara zilikuwa hazipitiki kutokana na nyingine kufungwa na kusababisha usumbufu mkubwa.
Waandishi nao matatani
Katika
vurugu hizo, baadhi ya waandishi wa habari walishambuliwa na polisi.
Hao ni pamoja na Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti la The Citizen,
Zephania Ubwani ambaye kabla ya kuchomoka katika mikono ya askari,
alikuwa akiwaonyesha kitambulisho chake cha kazi.
Hata hivyo, askari hao walimtishia kumtandika na kisha kumwambia aondoke katika eneo hilo kwa kuwa haijalishi yeye ni nani.
Mwingine
ni mwandishi wa gazeti la Nipashe, Cnythia Mwilolezi ambaye alilazimika
kuacha viatu na vitendea kazi vyake katika Uwanja wa Soweto na
kukimbilia kwenye moja ya nyumba zilizopo jirani na eneo la tukio.
Katibu
Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Moses Kilyinga
alipigwa na polisi baada ya kuonekana akichukua maelezo.
Kilyinga
ambaye alishambuliwa na askari hao alisema mara baada ya askari hao
kumkamata, alijitambulisha lakini hawakumwelewa na wakaendelea kumchapa
kabla ya kufanikiwa kuchomoka.
Polisi wavamia hospitali
Wakati
baadhi ya majeruhi wakidai kushuhudia polisi wakiwapiga risasi watu
waliokuwa wakimkimbiza mtu aliyerusha bomu katika tukio la Jumamosi,
askari hao juzi walifika katika Hospitali ya Seliani saa mbili usiku
wakitaka kumchukua mmoja wa majeruhi kwa mahojiano kuhusiana na tukio
hilo. Hata hivyo, hawakufanikiwa baada ya mgonjwa kutokomea
kusikojulikana baada ya kupata taarifa za kutaka kuhusishwa na tukio
hilo.
Ingawa
si polisi wala Chadema waliokuwa tayari kumtaja mgonjwa huyo, inaelezwa
kwamba majeruhi anayesakwa ni Abdallah Alila aliyekaririwa na vyombo
vya habari jana na juzi akidai kumshuhudia aliyerusha boma akiondoka
kwenye moja ya magari ya polisi.
Hata
hivyo, Kamishna Chagonja jana alisema kwamba jeshi lake linapenda
kushirikiana na raia kupata taarifa na si kutumia nguvu katika kukusanya
ushahidi wake.
No comments:
Post a Comment