Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, January 22, 2013

Kushadidi malalamiko ya wananchi wa Marekani dhidi ya Israel

Hasira za walimwengu dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel zinazidi kuongezeka huku utawala huo pandikizi na ulio dhidi ya ubinaadamu ukizidi kutengwa kimataifa. Wigo wa hasira hizo umepanuka hadi katika nchi za Magharibi na hususan Marekani ambako viongozi wake ni waungaji mkono wakubwa wa utawala wa Kizayuni. Wananchi wa Marekani wameshoshwa na siasa za viongozi wao za kuoanisha manufaa ya nchi hiyo na yale ya utawala wa Kizayuni na wamekuwa wakionyesha hasira zao kwa njia tofauti kupinga uungaji mkono wa kibubusa wa viongozi wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni. Mji wa Washington huko Marekani umekuwa uwanja wa malalamiko ya wananchi dhidi ya Israel. Wananchi wamefanya maandamano kuelekea Ikulu ya Marekani, White House ili kuwaonesha viongozi wa nchi hiyo upofu wa siasa zao kuhusu Israel.
Maandamano hayo yamefanyika sambamba na sherehe za kuapishwa Barack Obama kuwa Rais wa Marekani kwa kipindi cha pili mfululizo. Waandamanaji hao pia wametoa nara na kaulimbiu za kuwaunga mkono Wapalestina na kutaka Marekani iache kuiunga mkono Israel. Kitu kilichoongeza mvuto wa maandamano hayo ni kushiriki ndani yake wazazi wa Rachel Corrie, mwanaharakati wa Kimarekani aliyeuliwa na mabuldoza ya Israel huko Ghaza Palestina mwaka 2003. Baba wa mwanaharakati huyo wa kike raia wa Marekani aliwahutubia waandamanaji na kusema kuwa: Nimesimama hapa kiukumbusha serikali ya Marekani kwamba haipaswi kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni. Amesema, Wazayuni walimuua binti yake kwa kumkanyaga kwa mabuldoza huko Ghaza miaka 10 iliyopita wakati alipokuwa anajaribu kuwazuia jinai za Wazayuni za kuwavunjia Wapalestina nyumba zao. Kwa kweli viongozi wa Marekani wako tayari kuuunga mkono utawala wa Kizayuni kwa thamani yoyote ile hata kama damu za Wamarekani zitamwagika. Lakini wananchi wa Marekani wanazidi kuamka siku baada ya siku na malalamiko yao dhidi ya siasa za viongozi wao za kutumia mabilioni ya fedha za walipa kodi huko Marekani kuulinda na kuundesha utawala wa Kizayuni yameongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni. Wazayuni wanatumia silaha za Marekani kuendeleza jinai zao dhidi ya Wapalestina na hili nalo limekuwa likilalamikiwa vikali na makundi yanayopinga vita nchini Marekani. Ni hivi karibuni tu ambapo wananchi wa mji wa Seattle wa Marekani walikodi makumi ya mabasi ya umma na kubandika matangazo yanayopinga siasa za Marekani za kutumia fedha za wananchi wa nchi hiyo kuuendesha utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika siku za hivi karibuni pia, wanaharakati wa Vyuo Vikuu vya Marekani kama vile Ridgely Fuller wamekuwa wakidhihirisha waziwazi upinzani wao kuhusu siasa hizo za Marekani. Ukweli ni kwamba kuusaidia kijeshi utawala wa Kizayuni wa Israel ni jambo linalopingwa na hata sheria za Marekani kwenyewe ambazo zinapiga marufuku kutumwa misaada ya kijeshi kwa tawala ambazo zinatumia silaha na fedha za Marekani katika mashambulizi na ukandamizaji. Hata hivyo linapofika suala la utawala wa Kizayuni, viongozi wa Marekani hawajali sheria zote hizo na cha ajabu ni kuwa, utawala wa Kizayuni hautosheki na kila leo unashinikiza kupata misaada na uungaji mkono zaidi wa viongozi wa Marekani kwa jinai zake.

No comments: