Vyombo vya habari vimeripoti kuwa serikali ya Marekani imeamua
kuliondoa jina la kundi la kigaidi la Munafiqin MKO katika orodha ya
makundi ya kigaidi. Kanali ya habari ya BBC imelinukuu shirika la habari
la Reuters na kutangaza kuwa serikali ya Marekani imeamua kuliondoa
jina la kundi la kigaidi la Munafiqin MKO katika orodha rasmi ya makundi
ya kigaidi. Shirika hilo la habari limewanukuu viongozi rasmi wawili wa
Marekani kwa sharti la kutotajwa majina yao wakisema kuwa serikali ya
Washington imeamua kulifuta rasmi jina la kundi la kigaidi la Munafiqin
katika orodha ya makundi ya kigaidi ifikapo tarehe Mosi mwezi Oktoba
mwaka huu.
Kuhusiana na habari hiyo kumeashiriwa nukta hii kwamba
Hillary Clinton Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ametoa uamuzi
wa mwisho juu ya suala hilo. Marekani imeamua kulifuta jina la kundi la
kigaidi la Munafiqin yaani MKO katika orodha ya makundi ya kigaidi kwa
kisingizio cha kufungwa kambi ya Ashraf huko katika mkoa wa Diyala
nchini Iraq na kupigwa marufuku vitendo vya kigaidi vya kundi hilo tangu
mwaka 2003. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa mwezi Disemba mwaka
jana kati ya serikali ya Iraq na kundi la kigaidi la Munafiqin,
wanachama wa kundi hilo wanapaswa kuhamishiwa polepole katika kambi ya
Liberti na baada ya kufika hapo mazingira yaweze kuandaliwa kwa ajili ya
kuhamishwa tena wanachama hao na kupelekwa katika nchi nyingine. Hii ni
katika hali ambayo oparesheni ya kuwahamishia wanachama wa kundi la
kigaidi la Munafiqin katika kambi ya Liberti huko Baghdad imekamilika.
Kambi ya Liberti ilikuwa kambi kubwa zaidi ya Marekani huko Iraq ambayo
imekuwa ikitumiwa kwa muda na wanachama wa kundi la kigaidi la Munafiqin
baada ya vikosi vamizi vya Marekani kuondoka huko Iraq mwishoni mwa
mwaka jana. Jambo lililo wazi na lisiloweza kukanushika hapa ni kuwa
serikali ya Marekani inatumia maana ya neno 'mapambano dhidi ya ugaidi'
kwa maslahi yake katika kupambana na kundi la kigaidi la Munafiqin.
Njia inayotumiwa na serikali ya Marekani katika kuamiliana na kundi
hilo la kigaidi ni uthibitisho kamili wa maana ya ugaidi na migawiko
yake yaani ugaidi mzuri na mbaya kwa mtazamo wa viongozi wa Washington.
Radiamali ya serikali ya Marekani kwa vitendo vya kigaidi
vilivyofanywa na kundi la Munafiqin nchini Iran ambalo limewaua Wairani
elfu 12 inapaswa kuzingatiwa katika fremu ya migawiko ya ugaidi kwa
mujibu wa wa serikali ya Marekani yaani ugaidi mzuri na ugaidi mbaya.
Marekani na waitifaki wake wa Ulaya wamezusha chuki na uadui dhidi ya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na kusimama kwake imara mbele ya
siasa za mabavu na za kupenda kujitanua za nchi hizo. Kwa mtazamo wa
nchi hizo za Magharibi harakati yoyote iliyo dhidi ya Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran ikiwemo hata vitendo vitakavyosababisha kuuliwa shahidi
wanaume, wanawake na watoto wa Iran ni halali.
Kufungwa kambi ya Ashraf hakuwezi kuhalalisha kivyovyote kufutwa jina
la kundi la kigaidi lililokuwa limewekwa katika faharasa ya makundi ya
kigaidi. Yoyote aliyehusika kumwaga damu za maelfu ya watu wasio na
hatia anapasa kushtakiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo
serikali ya Marekani inafanya kila iwezalo ili kuzuia kusambaratika
kundi la Munafiqin la MKO ili kwa njia hiyo iweze kulitumia tena kundi
hilo katika vitendo vyake vya kuingilia masuala ya hapa nchini na ya
nchi nyingine za eneo. Kusalia au kufutwa jina la kundi la Munafiqin
katika orodha ya makundi ya kigaidi hakuwezi kubadilisha kivyovyote vile
sura chafu ya kundi hilo. Serikali ya Marekani imeamua kulifuta jina
la kundi la kigaidi la Munafiqin katika faharasa ya makundi ya kigaidi
ili kuhalalisha uungaji mkono wake kwa kundi hilo chini ya mwavuli wa
hatua za kibinadamu.
No comments:
Post a Comment