Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Friday, April 27, 2012

Charles Taylor wa Liberia apatikana na hatia The Hague

Mahakama Maalumu ya Sierra Leone iliyo na makao makuu yake huko The Hague nchini Uholanzi imempata na hatia ya jinai dhidi ya binadamu Charles Taylor, Rais wa zamani wa Liberia. Akikaribisha uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama hiyo, Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa uamuzi huo utakumbukwa kwa miaka mingi ijayo na watu wa Sierra Leone, Afrika na ulimwengu mzima kwa ujumla.

Taylor amepatikana na hatia ya kuwauzia silaha waasi wa Revolutionary United Front RUF wa Sierra Leone ambao wanatuhumiwa kuhusiaka na vitendo vya ugaidi, mauaji na ubakaji dhidi ya raia wasio na hatia katika kipindi cha vita vya ndani nchini humo. Waasi hao walinunua silaha kwa pesa ambazo zilitokana na mauzo ya almasi iliyochimbwa na watu waliolazimishwa kufanya kazi kama watumwa, almasi ambayo baadaye ilijulikana kwa jina la 'almasi ya damu.' Inasemekana Taylor alitaka kudhibiti migodi ya madini hayo kupitia waasi wa RUF. Kundi hilo la waasi linahesabiwa kuwa kundi lililoogopwa zaidi nchini Sierra Leone kati ya mwaka 1991 na 2002 kutokana na vitendo vyake vya kinyama dhidi ya raia. Kukata viungo vya mwili vya wapinzani na kutumia watoto kwenye maeneo ya vita pamoja na vitendo vingine vya mabavu dhidi wapinzani ni jambo lililokuwa la kawaida kabisa kutekelezwa na waasi hao. Mbali na Sierra Leone, Taylor anatuhumiwa kuwa chanzo muhimu cha kuzuka vita na machafuko nchini Liberia. Aliingia madarakani mwaka 1997 baada ya kuipinduia serikali ya Samuel Doe, jambo ambalo si tu kwamba halikusaidia kurejesha amani nchini bali lilichochea zaidi mivutano ya kisiasa na kupelekea nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kushuhudia moja ya vita vya muda mrefu zaidi barani humo. Katika vita hivyo makabila tofauti yalipigana kwa ajili ya kudhibiti maliasili muhimu za nchi hiyo. Vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa miaka 14 vilipelekea watu zaidi ya laki mbili kupoteza maisha na wengine karibu milioni moja kulazimika kuishi kama wakimbizi.
Baada ya kuangushwa serikali yake, Taylor alikimbilia Nigeria, ambapo Umoja wa Mataifa ulitoa amri ya kutiwa kwake mbaroni mwezi Juni mwaka 2003. Taylor alikamatwa mwezi Machi 2006 alipokuwa akijaribu kuvuka mpaka kuingia Cameroon na kukabidhiwa kwa Mahakama Maalumu ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Sierra Leone. Kesi yake ilianza tarehe 4 Juni 2007. Mahakama hiyo ilichunguza matukio yaliyotokea Sierra Leone mwaka 1996 hadi 2001 na wala
haikushughulikia jinai za vita ambazo huenda zilifanyika Liberia. Hukumu dhidi yake imepangwa kutolewa na mahakama hiyo mwishoni mwa mwezi Mei. Habari zinasema kuwa Taylor amepangiwa kufungwa katika mojawapo ya jela za mjini London Uingereza. Miaka mitano iliyopita serikali ya Uingereza iliahidi kumfunga jela nchini humo mtawala huyo wa zamani wa Liberia baada ya kupewa kifungo na mahakama iliyotajwa.

No comments: