Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Wednesday, May 14, 2014

Serikali ya Nigeria yakataa pendekezo la kundi la Boko Haram

Serikali ya Nigeria imekataa pendekezo lililotolewa na kundi la kigaidi la Boko Haram la nchi hiyo lililoitaka serikali ibadilishane nalo wanamgambo wa kundi hilo wanaoshikiliwa kwenye jela za serikali, na mabinti liliowateka nyara hivi karibuni. Huku akionyesha mkanda wa video wa mabinti kadhaa waliokuwa wakisoma Qur'ani, Abubakar Shekau kamanda wa wanamgambo wa Boko Haram amedai kuwa mabinti hao ni wale waliotekwa nyara na wanamgambo hao tarehe 14 Aprili huko katika mji wa Chibok ulioko katika jimbo la kaskazini mwa Nigeria la Borno. Ujumbe wa mkanda huo unasema kuwa mabinti hao ambao wote walikuwa Wakristo sasa wamesilimishwa na wanamgambo wa Boko Haram.
Abubakar Shekau ameiambia serikali kwamba yuko tayari kuwaachilia huru mabinti hao wote 223 iwapo serikali itawaachilia huru wanamgambo wa Boko Haram wanaoshikiliwa katika jela za serikali. Mabinti 276 walikuwa katika shule ya bweni ya Chibok ilipovamiwa na Boko Haram lakini baadhi yao walifanikiwa kukimbia na kuokoa maisha yao wakati wa kutekelezwa uvamizi huo. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa huenda pendekezo hilo la Boko Haram likakubaliwa na serikali baadaye iwapo litaonekana kuwa na maslahi kwa jamaa za mateka na serikali ya Abuja.
Shehu Sani mtaalamu kuhusiana na kundi la Boko Haram anasema kuwa washukiwa wanaofungamana na kundi la Boko Haram wanagawanyika katika makundi matatu ya makamanda wa ngazi za juu, askari wanamgambo na watu wa karibu pamoja na familia za makamanda wa Boko Haram. Sani anaamini kwamba huenda serikali ya Nigeria ikaliachilia huru kundi hili la tatu yaani wanawake na mabinti wa  watu wanaofungamana na Boko Haram ili kuonyesha nia yake njema kwa kundi hilo. Pendekezo kama hilo la kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa wa Boko Haram pia lilitolewa mwaka uliopita. Wakati huo, ni familia za watu wanaozungumza Kifaransa wa Kaskazini mwa Cameroon ndio waliokuwa wametekwa nyara na Boko Haram na ziliachiliwa huru baada ya kufanyika mazungumzo kati ya wawakilishi wa kundi hilo na gavana wa jimbo la Kano la Nigeria. Wakati huohuo, wataalamu wengine wa mambo wanasema kuwa pendekezo hilo la Abubakar Shakeu la kubadilishana mateka na wafungwa wa Boko Haram ni alama ya kulegeza msimamo wake wa hapo awali.
Tukio la kutekwa nyara wasichana waliotajwa wa shule na kundi la kigaidi la Boko Haram, tukio la kinyama ambalo limelaaniwa vikali na taasisi pamoja na serikali nyingi za dunia, ni jambo ambalo lilikuwa halijawahi kutekelezwa na kundi hilo tokea lianzishe mapambano ya silaha dhidi ya serikali ya Abuja mwaka 2009. Kwa kuzingatia uungaji mkono wa kimataifa kwa serikali ya Nigeria dhidi ya Boko Haram, huu ni wakati muafaka kwa serikali kupambana  vilivyo na kundi hilo na kuwathibitishia walimwengu upotofu wa fikra zake, kundi ambalo linalochafua jina la Uislamu kwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi dhidi ya watu wasio na hatia. Wataalamu wa mambo wanaamini kuwa kama serikali ya Nigeria haitachukua hatua za dharura na za haraka kwa lengo la kuwakomboa mabinti hao mateka bila shaka jambo hilo litaandaa uwanja mzuri kwa ajili ya nchi za Magharibi kama vile Ufaransa, Uingereza na Marekani kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo. Kwa sasa nchi hizo zinautazama utajiri mkubwa wa maliasili wa Nigeria kwa jicho la tamaa na kwa hivyo ziko tayari kutumia kisingizio chochote kile kupora utajiri huo kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.

No comments: